Raila chaguo la Uhuru 2022 – Murathe

Na WANDERI KAMAU

KUNA uwezekano wa Rais Uhuru Kenyatta kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuwania urais 2022, licha ya tashwishi ambazo zimeonekana kukumba handisheki katika siku za hivi karibuni.

Kulingana na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, Bw Odinga ndiye mwanasiasa pekee mwenye uwezo, ushawishi na ufuasi mkubwa kisiasa kumkabili Naibu Rais William Ruto, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Bw Murathe ni miongoni mwa washirika wa karibu zaidi wa Rais Uhuru Kenyatta na kauli zake zimekuwa zikifasiriwa kuwa “sauti” ya rais.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumapili usiku, Bw Murathe alipuuzilia mbali muungano wa One Kenya Alliance (OKA), akisema wanachama wake hawana ushawishi ufaao kisiasa kumkabili Dkt Ruto.

Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

“Lengo letu ni kuhakikisha (Dkt Ruto) hashindi urais hata kidogo 2022. Kwa mkakati huo, mwanasiasa pekee mwenye uwezo kutimiza hilo ni Bw Odinga. Ana ufuasi katika karibu nusu ya nchi. Huwezi kumpuuza kisiasa hata kidogo,” akasema.

Kauli yake inajiri wakati kumekuwa na tashwishi miongoni mwa washirika wa Bw Odinga katika ODM, kuhusu ikiwa huenda Rais Kenyatta na waandani wake wanamfunga macho kisiasa kupitia handisheki.

Hofu hiyo iliibuliwa na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo mwezi uliopita, alipodai kwamba baadhi ya washirika wa Rais Kenyatta walikuwa wakijaribu kumzima kisiasa Bw Odinga, kwa kupanga kisiri kuhusu mchakato wa urithi wake.

“Inasikitisha wakati Rais Kenyatta na Bw Odinga wanaendelea na mikakati ya kuipigia debe ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), kuna kundi la maafisa wakuu serikalini wanaopanga kuhusu namna Kenya itatawaliwa baada ya rais kung’atuka,” akasema Bw Orengo.

Kauli hiyo ilifuatwa na uvumi kuhusu uwezekano wa Bw Odinga na Dkt Ruto kubuni muungano wa kisiasa, hali inayotajwa kuzua wasiwasi wa kisiasa katika kambi ya Rais Kenyatta.

Hayo yanatajwa pia kuchangiwa na madai kuwa Rais Kenyatta anaupendelea muungano wa OKA kuliko ushirikiano uliopo baina yake na Bw Odinga.

Ni hali iliyowafanya washirika wa Rais Kenyatta kufanya msururu wa mikutano, kumhakikishia Bw Odinga kwamba handisheki ingali thabiti.

Hata hivyo, Bw Murathe alisisitiza kuwa kando na umaarufu wake, Bw Odinga ndiye anayefaa zaidi kuwa rais, kwani ameonyesha uzalendo na uvumilivu mkubwa hata baada ya tofauti za kisiasa kuibuka kati yake na Rais Kenyatta na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

“Bw Odinga ni mwanasiasa ambaye ameonyesha uzalendo wa kweli. Alikubali kubuni serikali ya muungano na Bw Kibaki ili kuleta uthabiti wa kisiasa nchini baada ya ghasia za 2007. Vile vile, alikubali kubuni handisheki na Rais Kenyatta 2018 baada ya utata uliokumba uchaguzi wa 2017 ili kurejesha amani nchini,” akasema.

Wakati huo huo, alieleza mchakato wa vyama vya Jubilee na United Democratic Alliance (UDA) kutengana rasmi kisiasa utafanyika wiki hii.

UDA ilikuwa miongoni mwa vyama washirika vya Jubilee kama Party for Reforms and Development (PDR), lakini ikabadilishwa jina na waandani wa Dkt Ruto.

Habari zinazohusiana na hii

Walioingia mitini

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA