• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
NASAHA ZA RAMADHAN: Tusipoteze fursa ya kutaka msamaha kwa dhambi zetu

NASAHA ZA RAMADHAN: Tusipoteze fursa ya kutaka msamaha kwa dhambi zetu

Na KHAMIS MOHAMED

KWA kawaida binadamu anajulikana ni mwenye kutenda madhambi.

Hakuna binadamu aliyesalimika na sifa hii ya kuwa mwenye kukosa mara kwa mara.

Kwa sababu hii, Mwenyezi Mungu kutokana na kuwa mwingi wa huruma kwa waja wake, amefungua na kuiweka wazi milango yote ya toba kila wakati, haswa katika msimu huu wa Ramadhani.

Katika aya nyingi za Qurani, Mwenyezi Mungu anawapa matumaini ya msamaha na rehema watenda dhambi.

Katika Suratu Zumar aya ya 53 Mwenyezi Mungu anasema: “Sema: Enyi waja wangu mliojidhulumu wenyewe! Msikate tamaa na rehema za Mwenyezi Mungu. Bila shaka Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”

Mwenyezi Mungu anawasisitizia watenda dhambi kwamba, hawatakiwi kukata tamaa kwa msamaha wa Mwenyezi Mungu kwani kitendo hicho cha kukata tamaa, ni dhambi kubwa.

Kwa sababu hiyo dini, ya Kiislamu imefungua milango ya matarajio kwa ajili ya msamaha wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Katika Kumi la pili la mwezi mtukufu wa Ramadhan ambalo ni kumi la Maghfira, Waislamu wanatarajia kupata msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Yatupasa tuombe toba kwa makosa tuliyofanya. Yatupasa kuzidisha ibada sana ili tuwe miongoni mwa wale watakao samehewa

Wasomi wa Kiislamu wanasema kwamba toba ni faradhi kwa kila mwanadamu kulingana na mafunzo ya dini.

Mtume Muhammad (S.A.W) naye anatueleza faida ya kufanya Istighfaar kama ilivyo simuliwa na Hadhrat Abbaas [ra] kwamba Mtume [saw] alisema: Yule mtu anayeshikamana na Istighfaar, Mwenyezi Mungu Humtengenezea njia ya kutoka kwenye kila dhiki.

Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya faraja toka kwenye kila shida na humpatia riziki katika njia zile ambazo hata hawezi kuzidhania.

Ewe Mwenyezi Mungu hakika wewe Ni Msamehevu unapenda kusamehe, basi twaomba utusamehe.

Ewe Mwenyezi Mungu ulituambia wewe ni msamehevu. {Waambie Waja Wangu ya Kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.} (Alhijr: 49).

Tuhurumie Na tusamehe Ewe Mwenye maghfira tupe nguvu ya kufanya Istighfaar na kutubia madhambi yetu haswa katika mwezi huu wa toba, mwezi wa Ramadhani.

You can share this post!

Wamiliki hoteli wapinga ushuru wa vitanda

Wakuzaji miwa walia hatua ya viwanda itawaletea hasara