• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wakuzaji miwa walia hatua ya viwanda itawaletea hasara

Wakuzaji miwa walia hatua ya viwanda itawaletea hasara

Na GEORGE ODIWUOR

WAKULIMA wa miwa katika kaunti za Migori na Homa Bay, wanahofia hasara kubwa, baada ya usimamizi wa kampuni za kusaga miwa kufeli kutii maafikiano ya awali ya kukata miwa hiyo shambani na kuisafirisha isagwe viwandani.

Zaidi ya wakulima 500 kutoka Migori na Homa Bay wanadai kwamba hatua ya viwanda vya sukari vya Sony, Transmara na Sukari kughairi makubaliano ya awali, itawasababishia hasara kubwa kifedha.

Badala yake wakulima hao sasa wanadai viwanda hivyo vinaendea miwa kutoka kaunti nyingine huku miwa katika ekari kadhaa za ardhi Homa Bay na Migori zikiendelea kuharibika kwa kukosa kukatwa na kupelekwa kiwandani kwa wakati.

Miezi michache iliyopita, wakulima na usimamizi wa viwanda, walikubaliana kwamba miwa kutoka kwa wakulima wa kaunti hizo tatu itakatwa na kusafirishwa kiwandani ili kuzuia uharibifu wa kila mwaka wa mavuno.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wakulima wa Miwa, Bw Era Okoth, alisema kuwa miwa katika mashamba mengi imekomaa na inaelekea kupita kiwango cha kukatwa huku akidai viwanda vingi sasa vinategemea miwa kutoka Kisumu.

“Masaibu yetu yanasababishwa na hatua ya viwanda kugeuka ghafla na kupuuza makubaliano yetu ya awali ambayo yangewezesha miwa yetu kupewa kipaumbele,” akasema Bw Okoth.

Kutokana na hatua hiyo, wakulima wa miwa sasa wametishia kuelekea mahakamani kama njia ya kulazimisha usimamizi wa viwanda kuagiza miwa yao iondolewe mashambani na kusagwa viwandani.

Aidha Bw Okoth amewataka viongozi kutoka Migori na Homa Bay waangazie suala hilo na kuwatetea wakulima ili suala hilo lishughulikiwe.

“Viwanda hivyo havifai kununua miwa kutoka kwa kaunti nyingine kwa muda wa miezi mitatu hadi miwa ya Homa Bay na Migori iondolewe mashambani kisha kusagwa,” akasema Bw Okoth.

Pia kutokata miwa kwa wakati katika Kaunti ya Homa Bay kumechangiwa na hali mbaya ya barabara hasa wakati huu mvua inapoendelea kushuhudiwa.

Wakulima wamelaumu utawala wa kaunti kwa kukosa kukarabati barabara licha ya kuwatoza ada ya usafirishaji wa miwa kila mara.

Wakulima kutoka Ndhiwa nao wametishia kuandaa maandamano makubwa dhidi ya serikali ya Kaunti ya Homa Bay ili kuishinikiza ikarabati barabara hiyo.

“Kaunti hututoza ada kila mara ili kutengeneza barabara. Tunataka kujua pesa hizo huenda wapi licha ya barabara kuendelea kuwa katika hali mbaya,” akasema mkulima kutoka Ndhiwa Vitalis Okinda.

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHAN: Tusipoteze fursa ya kutaka msamaha kwa...

Ucheleweshaji wa matokeo waathiri vita dhidi ya Covid