• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
TAHARIRI: Serikali izingatie ripoti za watafiti

TAHARIRI: Serikali izingatie ripoti za watafiti

KITENGO CHA UHARIRI

SERIKALI haifai kupuuza tafiti zinazotelewa na mashirika mbalimbali kuhusu mwelekeo wa taifa hasa wakati huu uchumi umeathirika na maisha ya raia kusambaratishwa kutokana na uwepo wa janga la virusi vya corona.

Mnamo Jumapili Shirika la Utafiti la Infotrak lilitoa matokeo yaliyoonyesha kwamba zaidi ya nusu ya Wakenya wanahisi taifa lipo kwenye mkondo mbaya kutokana na maisha magumu wanayoyapitia.

Kati ya mambo makuu ya sasa yanayowatatiza Wakenya hasa ni gharama ya juu ya maisha, ukosefu wa ajira na janga la corona ambalo halijatikisa Kenya pekee bali ulimwengu mzima.

Masuala mengine yaliyowakera Wakenya yaliyotajwa na Afisa Mkuu wa Shirika hilo Angela Ambitho ni ufisadi uliokita mizizi serikalini pamoja na nchi kuendelea kupata mikopo mikubwa kutoka kwa mashirika ya kifedha duniani kama IMF.

Kimukhtasari, Wakenya wengi wamelemewa na hali ya maisha ya sasa na utafiti huo unaafiki kabisa. Hata hivyo, swali kuu ni je, serikali huwa inatathmini tafiti hizi zinazohusisha Wakenya na kuwajibikia masuala yaliyoibuliwa?

Mara nyingi tafiti hizi huanika udhaifu wa serikali lakini ni vyema kwamba masuala yanayoibuliwa yaangaziwe na kutafutiwa suluhu. Kwa mfano suala la ukopaji wa kila mara linaanika jinsi ambavyo mzigo wa deni nchini unaendelea kupanda ilhali pesa hizo huishia mikononi mwa watu wachache kutokana na ufisadi uliokita mizizi kiasi kwamba Rais Uhuru Kenyatta amewahi kusema hadharani nchi hupoteza Sh2 bilioni kila siku.

Vilevile, suala la ajira limekuwa likiibuliwa katika tafiti nyingi wala si Infotrak pekee. Hata hivyo, utawala wa Jubilee ulioahidi kubuni nafasi nyingi za kazi haujafanya chochote cha kutimiza hilo na badala yake huzingirwa tu na ushindani wa kisiasa kati ya mirengo miwili.

Badala ya serikali kuona kama mashirika haya ya serikali yanaanika udhaifu wake na ni adui, inafaa ishirikiane nao kuhakikisha kuwa masuala hayo yanayowakumba Wakenya yanatatuliwa.

Kutokana na tafiti zinazoendelea kutolewa ni wazi maisha ya Wakenya yameathirika na janga la corona, na ni vyema iwapo serikali itakumbatie mbinu za kuwasaidia ili warejelee maisha yao ya awali.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Hoteli inayosaidia watalii kuelewa ramani ya...

ODONGO: Kwa kumpinga Raila, Obado anajiua kisiasa