• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
WANGARI: Uteuzi wa jaji mkuu mpya utekelezwe kwa makini

WANGARI: Uteuzi wa jaji mkuu mpya utekelezwe kwa makini

Na MARY WANGARI

WAKENYA wamekuwa wakifuatilia kwa makini shughuli ya kumteua Jaji Mkuu mpya ambayo ilianza mapema wiki iliyopita.

Mchakato huo wa kuwapiga msasa wagombea 10 wanaojumuisha wanaume 7 na wanawake watatu, umeibua masuala mengi muhimu kando na kumsaka bosi mpya wa Idara ya Mahakama (JSC) nchini.

Jopo la makamishna tisa wa JSC limekuwa likiwatoa kijasho na hata kuwafanya baadhi ya wahojiwa kutiririkwa na machozi kwa maswali yao makali.

Sehemu kubwa ya mchakato huo imekuwa ikitathmini ujuzi kielimu, kitaaluma, tajriba, uelewa wa masuala ya kisheria na hata baadhi ya maamuzi katika kesi za awali.

Huku shughuli ya kumsaka mrithi wake jaji mkuu mstaafu David Maraga ikiendelea wiki hii, suala tata linalojitokeza ni kuhusu nia hasa ya mchakato huo.

Je, unalenga kuboresha maslahi ya raia au ni njama nyingine tu za vyombo vya dola kukidhi na kulinda maslahi ya kisiasa?

Huku ikiwa imesalia miezi kadhaa tu kabla ya Uchaguzi Mkuu 2022, ni vigumu kubaini lengo halisi la mchakato huo huku kumbukumbu za uhusiano tata kati ya aliyekuwa jaji mkuu na serikali zikisalia.

Hii ni baada ya Maraga kufutilia mbali uchaguzi mkuu wa 2017 katika uamuzi wa kwanza wa aina hiyo kuwahi kufanyika Kenya.

Jaji mkuu huyo mstaafu atakumbukwa mno kwa ujasiri wake wa kuikosoa serikali hadharani jambo lililozorotesha zaidi uhusiano kati yake na utawala.

Ni kwa sababu hiyo ambapo mchakato huu wa kumteua jaji mkuu mpya unajitokeza kama mchezo wa karata ambapo wahusika wakuu wanatathmini kwa makini kila hatua wanazochukua.

Katika mchakato huu vilevile, kuna uwezekano wa mwanamke wa kwanza kuwa jaji mkuu nchini Kenya.

Kwa mara ya kwanza kihistoria, wanawake watatu wenye ujuzi na tajriba ya kujivunia wamejitokeza kukabiliana na wanaume katika kinyang’anyiro cha wadhifa huo nchini.

Bila shaka, umma unasubiri kwa hamu kuona atakayechaguliwa katika afisi hiyo inayomezewa mate ambapo nusu ya wagombea kufikia sasa, tayari wamepigwa msasa.

Umuhimu wa afisi ya jaji mkuu hauwezi ukasisitizwa vya kutosha hasa ikizingatiwa kuwa JSC ni kiambajengo kikuu katika utawala na kudumisha demokrasia nchini.

Kando na kulinda uhuru wa Idara ya Mahakama ili kuhakikisha majaji wanatoa maamuzi huru, jaji mkuu ana wajibu wa kuweka kanuni za kitaaluma zinazotoa mwongozo kuhusu utendakazi wa Idara hiyo.

Shughuli ya kudumisha viwango bora vya utendakazi katika taasisi yoyote ile ni wajibu muhimu unaopaswa kuchukuliwa kwa uzito unaostahili.

Ni sharti JSC iwe makini ili kuhakikisha jaji mkuu mpya atakayechaguliwa, awe mwanamke au mwanamme, ni mtu atayelinda hadhi ya idara hiyo ili kuvutia imani ya wananchi kuhusu mfumo wa haki nchi.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Kwa kumpinga Raila, Obado anajiua kisiasa

Waume wazomea pasta wa wake wao