Waume wazomea pasta wa wake wao

Na TOBBIE WEKESA

INGOTSE, KAKAMEGA

MAKALAMENI kadhaa waliwashangaza wengi walipovamia mkutano wa wahubiri wa eneo hili wakidai wake wao wamepotelea makanisani.

Duru zinasema kwamba makalameni hao walevi waliweka wazi changamoto ambazo wanapitia wafikapo nyumbani na kuwakosa wake wao.

“Kila wakati nikifika kwangu huwa simpati mke wangu. Nikiuliza alikoenda naambiwa yuko kanisani. Huduma gani inafanywa hadi jioni,” polo mmoja alifoka.

Mapasta waliohudhuria walisikiliza malalamishi ya majamaa hao kwa makini. Jamaa hao walidai kwamba wakati mwingine wanalazimika kushinda kwa mamapima hadi usiku kwa sababu wake wao wamepotelea makanisani.

“Sisi sote tulioitisha mkutano huu tunajuana. Baada ya hapa tunaenda kwa mamapima kupewa roborobo. Mamapima ndio wanaotushughulikia kila kitu,” polo alifoka.

Mapasta waliwaahidi makalameni hao kwamba watashughulikia madai yao.

“Tumesikia tetesi zenu. Tutawashauri wake zenu wawe wakirudi mapema,” pasta mmoja alieleza.

Duru zinadai makalameni hao hawakuridhika na maelezo ya pasta.

“Mimi nimechoka kukaa njaa na nina mke. Nyinyi mapasta ninaona vitambi mnazidi kujaza. Wake zenu wanawahudumia lakini wetu wanaishi makanisani mwenu,” mlevi mwingine alifoka.

Inadaiwa jamaa hao waliwaamru mapasta kutowaruhusu wake wao kushinda kanisani kwa muda mrefu.

“Hatusemi wasiombe lakini msikae nao sana. Wakishawahudumia waamrisheni waje watuhudumie sisi pia la sivyo tutafungua makanisa yetu,” mlevi mwingine alifoka.

Penyenye zinasema baada ya kikao makalameni walifuatana hadi kwa mamapima huku mapasta wakienda zao.

“Nikirudi jioni nimkose mke wangu walahi Jumapili nitavuruga shughuli katika kanisa analoshiriki. Hii tabia imezidi,” polo mmoja alifoka na kuungwa mkono na wenzake.

Haikujulikana iwapo mapasta waliwashauri wanawake kuwa wakirudi makwao mapema au walipuuza vilio na vitisho vya makalameni hao.