• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Omala ajiandaa kwenda Uswidi kusakatia Linkoping City

Omala ajiandaa kwenda Uswidi kusakatia Linkoping City

Na JOHN ASHIHUNDU

MSHAMBULIAJI chipukizi Benson Omala wa Gor Mahia sasa amepata kibali rasmi cha kuanza kuchezea klabu ya Linkoping City nchini Uswidi.

Omala ambaye alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliomaliza mtihani wao wa Kidato cha Nee ameeleza furaha yake baada ya kupata cheti cha kufanya kazi nchini Uswidi.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Western Stima amejiunga na klabu hiyo ya Daraja la Kwanza kwa mkataba wa miezi sita. Mkataba huo utamalizika Disemba 21, atakaporejea katika klabu yake ya Gor Mahia.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 18 alisema tayari ameanza mipango ya kuondoka nchini kuelekea Uswidi.

“Cheti changu cha kusafiria kipo tayari, na sasa nitaondoka wakati wowote. Jukumu langu kwa sasa ni kusakata soka ya kulipwa barani Ulaya huku nikingojea matokeo ya mtihani,” alisema Omala.

“Nimekuwa nikifuatilia mechi za Linkoping na kufikia sasa wamecheza mechi tatu. Katika umri wangu mdogo, ningependa nifaulu katika soka ya kulipwa kama watangulizi wangu kama Victor Wanyama na Michael Olunga,” aliongeza.

Lonkping wamepoteza mechi zote tatu za kwanza- dhidi ya Varnesborg, Torns na Utsikten- katika Daraja la Kwanza ligini.

Omala ambaye alikuwa mwanafunzi katika shule ya upili ya Kisumu Day, alisema hakuweza kucheza mechi nyingi kutokana na shughuli za masomo.

“Nawatakia Gor Mahia kila la heri katika mechi zao, huku nikiwapongeza kwa kunipa nafasi kucheza mechi za Klabu Bingwa barani Afrika dhidi ya APR ya Rwanda.”

Katibu wa Gor Mahia, Sam Ochola alithibitisha kwamba Omala atarejea nyumbani mapema mwaka 2022 mara tu mkataba wake utakapomalizika mwezi Disemba.

You can share this post!

‘Usilaze damu mwanamke wewe’ 

Mwanatenisi Okutoyi atupwa chini nafasi sita, anashikilia...