• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Wadau waidhinisha mpango wa kupanua ushiriki wa UEFA kutoka timu 32 hadi 36 kuanzia 2024

Wadau waidhinisha mpango wa kupanua ushiriki wa UEFA kutoka timu 32 hadi 36 kuanzia 2024

Na MASHIRIKA

PENDEKEZO ya kupania ushiriki wa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kutoka timu 32 hadi 36 limeidhinishwa.

Kuidhinishwa kwa pendekezo hilo kunajiri siku moja baada ya vikosi 12, vikiwemo sita vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutangaza mpango wa kujiunga na kivumbi kipya cha European Super League (ESL).

Kwa mujibu wa vinara wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa), mfumo mpya wa kipute kilichopanuliwa cha UEFA utaanza kutekelezwa mnamo 2024 na utaendeshwa hadi 2033.

Kabla ya kujiuzulu wadhifa wake mnamo Machi, aliyekuwa mwenyekiti wa Shirikisho la Klabu za bara Ulaya (ECA), Andrea Agnelli, alisema mwafaka kuhusu jinsi nafasi nne za ziada zitakavyogawanywa miongoni mwa mataifa wanachama utafichuliwa chini ya “kipindi cha wiki chache zijazo”.

Kupanuliwa kwa ushiriki wa UEFA kunatarajiwa kuzima mchakato wa kutekelezwa kwa kipute kipya cha European Super League (ESL) ambacho kimepingwa vikali na mashabiki wa soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Katibu Mkuu wa Uefa, Giorgio Marchetti pamoja na vinara wa Euro na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

“Umoja wetu utasambaratishwa iwapo baadhi ya mawazo yatakumbatiwa kwa misingi potoshi ya kuvumisha maendeleo ya soka na kufanya mchezo huo kuwa kiwanda cha ajira na kitega-uchumi kwa wachezaji wa mataifa mbalimbali,” akasema Marchetti.

Ingawa hivyo, maoni yake yalitofautiana pakubwa nay a Agnelli ambaye pia ni mwenyekiti wa kikosi cha Juventus kinachoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Mpango wa kupanuliwa kwa ushiriki wa kipute cha UEFA ni wazo asili la aliyekuwa kipa matata wa Manchester United, Edwin van der Sar ambaye kwa sasa ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kikosi cha Ajax nchini Uholanzi.

Iwapo mfumo mpya utaidhinishwa, basi badala ya makundi manane ya awali yaliyojumuisha vikosi vinne vya kila kundi vikisakata mechi sita, sasa timu zote zitatandaza mechi 10 dhidi ya nyingine baada ya kupangwa kulingana na uwezo, nguvu na msimamo wao kwenye orodha ya viwango bora vya Uefa.

Matokeo ya mechi hizo zote yataamua msimamo wa jedwali ambapo sasa mechi za mikondo miwili zitapigwa na kila kikosi kuamua washindi watakaofuzu kwa hatua ya mchujo itakayoandaliwa kila baada ya Krismasi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Zamu ya Fred Ngatia mbele ya jopo la JSC kwenye mchakato wa...

Seneti yaondolea KNH lawama kuhusu kifo cha Walibora mauko...