• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Wakazi wa Thika kunufaika na umeme mitaani

Wakazi wa Thika kunufaika na umeme mitaani

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI  watanufaika na mpango wa kuweka umeme katika mitaa yote Thika na vitongoji vyake.

Kaunti ya Kiambu imejitolea kuona ya kwamba wakazi wa maeneo hayo wanapata umeme ili kuendesha biashara zao bila shida.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, alitoa hakikisho hivi majuzi kuwa miradi yote inayoendelea maeneo tofauti itakamilika jinsi ilivyopangwa.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba tunakamilisha miradi yote iliyopendekezwa katika kaunti nzima ya Kiambu. Kila mfanyakazi aliyepewa jukumu la kutekeleza wajibu wake ni sharti afanye bila kusita,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema wakati huu hakuna haja ya kuhubiri siasa chafu bali ni kuchapa kazi kwani “tumesalia na mwaka mmoja na nusu uchaguzi ufike”.

Aliyasema hayo wiki jana alipozuru mji wa Thika ili kujionea mwenyewe jinsi umeme katika mitaa unavyosambazwa.

Alitoa changamoto kwa madiwani wafanye juhudi kuona ya kwamba wanawatumikia wananchi walioko mashinani.

“Wakati wa kuzozana ulikwisha na sasa wananchi wanataka kuona maendeleo ili waridhike na kazi tunayofanya,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema wakati huu wa kupambana na janga la Covid-19, wananchi wanastahili kuwa makini na kufuata maagizo yote yaliyowekwa na Wizara ya Afya.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alipongeza juhudi zilizochukuliwa na Kaunti ya Kiambu kwa sababu wafanyabiashara wanaendesha biashara yao kwa utulivu huku pia uhalifu ukiwa umepungua kwa sababu ya umeme.

“Tunajua sisi kama wafanyabiashara ni sharti tufanye kazi kwa utaratibu na serikali ya kaunti ili biashara ziweze kuimarika. Pia tutazidi kushirikiana nao ili kufanikisha malengo yetu ya kibiashara,” alisema Bw Wanyoike.

Alisema siku chache zijazo atafanya mkutano na washika dau wote wa kibiashara ili kuelewa matakwa yao ni yapi.

“Naelewa kwa muda mrefu kumekuwa na maswala mengi ambayo hayakuwa yametatuliwa kwa ushirikiano na kaunti ya Kiambu. Sasa tutaweza kulainisha mambo,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wito kwa walemavu wajiunge na miradi ya maendeleo

Rigathi Gachagua adokeza mkataba wa Mlima Kenya kumuunga...