• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Malalamiko ya MCK kwa DCI

Malalamiko ya MCK kwa DCI

Na CHARLES WASONGA

BARAZA la Kusimamia Vyombo vya Habari Nchini (MCK) limekashifu hatua ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuwaamuru wanahabari wa shirika la habari la Royal Media Services (RMS) kufika mbele yao kudadisiwa kuhusu makala yaliyosema polisi hukodisha bunduki kwa wahalifu.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Afisa Mkuu Mtendaji wa MCK David Omwoyo alisema hatua hiyo ni tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari na hivyo ni kinyume cha Katiba.

“Huku MCK ikitambua wajibu wa DCI, inatarajiwa wajibu huo uelekezwe katika kuchunguza suala hilo bali sio kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari kujieleza na kupata habari unaolindwa na vipengele 33, 34 na 35 vya Katiba,” akasema Bw Omwoyo.

Akaongeza: “Kwa hivyo, ikiwa vyombo vya habari vinafichua maovu fulani miongoni mwa maafisa fulani katika Idara ya Polisi, sio haki kwa idara hiyo kutaka kuwachunguza wanahabari au kuwaagiza kufika mbele ya maafisa wake.”

Afisa huyo wa MCK badala yake alipendekeza kuwa DCI inapaswa kuelekeza juhudi katika kuchunguza sababu zilizochangia maafisa wa polisi kukodi silaha kwa wahalifu.

Mnamo Jumatano, Bw Kinoti aliagiza Mkurugenzi wa Uhariri katika RMS Joe Ageyo, mwenzake anayesimamia mikakati Linus Kaikai na maripota kadhaa kutoa maelezo ya kina kuhusu makala “Bunduki Mitaani/ Gun Galore” yaliyoangazia visa vya maafisa wa polisi kukodi bunduki kwa wahalifu.

Makala hayo yalipeperushwa katika runinga ya Citizen mnamo Jumapili, Aprili 18, na mwanahabari mpekuzi Purity Mwambia, pia yalifichua sakata ambapo maafisa wa polisi hukodi pingu na sare zao kwa ada ndogo ya hadi Sh1,000.

Lakini Jumatano Bw Kinoti alipuuzilia mbali madai hayo akisema bunduki aina ya AK47 na bastola ndogo “sio mali ya polisi wa Kenya.”

“Hii bunduki inatoka China na haina nambari za utambulisha (serial numbers) za Kenya. Bastola hii ndogo inatoka Uturuki na binafsi sijawahi kuiona tangu nilipoanza kuhudumu katika Idara ya polisi,” Bw Kinoti akawambia wanahabari katika makao makuu ya DCI, Nairobi.

Silaha hizo, pingu na magwanda mengine ya polisi yaliwasilishwa kwa kituo cha polisi cha Kilimani na Bw Kaikai. Alisema zilipatikana na Bi Mwambia katika uchunguzi wake uliodumu kwa mwaka mmoja.

Bw Kinoti alitetea hatua yake ya kuwaagiza wahariri wa RMS kufika mbele yao akisema watapewa fursa ya kuangazia suala hilo kwa kina “bila kulazimishwa kufichua walikopata habari kuhusu sakata hiyo.”

“Hatujui ni uhalifu aina gani ambao huenda ulitekelezwa kwa silaha hizi. Tutawataka wahariri hao watusaidie kupata kiini cha suala hili,” akasema.

Lakini Bw Omwoyo anashauri kwamba ikiwa DCI na idara ya polisi kwa ujumla inahisi kukerwa na makala hayo, wangewasilisha malalamishi yao kwa Kamati ya Kusikiliza Malalamishi kuhusu Vyombo vya Habari.

“Asasi hii ndiyo yenye mamlaka ya kushughulikia masuala kama haya kwa mujibu wa sehemu ya 27 ya Sheria ya MCK,” akasema.

Hata hivyo, Bw Kinoti alisema asasi husika katika idara ya polisi imewasilisha malalamishi katika kitengo hicho cha MCK.

You can share this post!

Timbe kutafuta mwanzo mzuri nyumbani Vissel Kobe na...

Ngatia atenga uhusiano wake na Rais akisaka kazi