• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 2:18 PM
FRENCH CUP: PSG yaingia nusu-fainali baada ya kuponda Angers 5-0

FRENCH CUP: PSG yaingia nusu-fainali baada ya kuponda Angers 5-0

Na MASHIRIKA

FOWADI Mauro Icardi alifunga mabao matatu na kusaidia waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) kuwakomoa Angers 5-0 uwanjani Parc des Princes mnamo Jumatano usiku.

Ushindi huo uliwezesha PSG ya kocha Mauricio Pochettino kutinga ndani ya nusu-fainali za French Cup kirahisi.

Icardi ambaye ni raia wa Argentina, aliwaweka PSG kifua mbele kunako dakika ya tisa baada ya kukamilisha krosi ya Julian Draxler. Vincent Manceau wa Angers alijifunga katika dakika ya 23 kabla ya Neymar Jr kuwapachikia PSG goli la tatu kunako dakika ya 65.

Icardi alicheka na nyavu za wageni wao kwa mara nyingine katika dakika za 68 na 90 baada ya kushirikiana vilivyo na mshambuliaji Angel Di Maria.

Mbali na kujiweka pazuri kutia kapuni taji la French Cup, PSG wanafukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Hali hiyo inamweka Pochettino katika nafasi nzuri ya kunyanyulia waajiri wake jumla ya mataji matatu katika msimu wake wa kwanza wa ukocha ugani Parc des Princes.

Kufikia sasa, PSG ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Manchester City kwenye nusu-fainali za UEFA, wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 kwa alama 69, moja pekee nyuma ya viongozi Lille.

PSG watavaana na Man-City katika mkondo wa kwanza wa hatua ya nne-bora ya UEFA mnamo Aprili 28 nchini Ufaransa kabla ya kushiriki marudiano mnamo Mei 4, 2021 nchini Uingereza.

Pochettino ambaye ni kocha wa zamani wa Southampton na Tottenham Hotspur, alipokezwa mikoba ya PSG mnamo Januari 2021 baada ya kutimuliwa kwa mkufunzi Thomas Tuchel ambaye kwa sasa anawatia makali masogora wa Chelsea ambao watapepetana na Real Madrid kwenye nusu-fainali nyingine ya UEFA msimu huu.

Tuchel alipigwa kalamu kambini mwa PSG licha ya kuongoza miamba hao wa soka ya Ufaransa kutwaa taji la Ligue 1 na French Cup pamoja na kutinga fainali ya UEFA ambapo walizidiwa ujanja na Bayern Munich ya Ujerumani iliyowapokeza kichapo cha 1-0 jijini Lisbon, Ureno.

Mbali na PSG, vikosi vingine ambavyo vimefuzu kwa nusu-fainali za French Cup muhula huu ni Montpellier, AS Monaco waliowacharaza Olympique Lyon 2-0 mnamo Aprili 21, 2021 na Vallieres wanaoshiriki Ligi ya Daraja la Nne nchini Ufaransa.

MATOKEO YA FRENCH CUP (Aprili 21, 2021):

PSG 5-0 Angers

Lyon 0-2 Monaco

You can share this post!

Kenya, DRC zatia saini mikataba ya kuimarisha ushirikiano

Polisi ashtakiwa kwa kuitisha hongo kutoka kwa mhudumu wa...