• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Inter Milan sasa pua na mdomo kutwaa taji la Serie A kwa mara ya kwanza tangu 2009-2010

Inter Milan sasa pua na mdomo kutwaa taji la Serie A kwa mara ya kwanza tangu 2009-2010

Na MASHIRIKA

LICHA ya kulazimishiwa sare ya 1-1 kutoka kwa Spezia mnamo Jumatano, Inter Milan walifungua pengo la alama 10 kileleni mwa jedwali na kuanza kunusia taji la kwanza la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) tangu msimu wa 2009-10.

Mshambuliaji Diego Farias aliwaweka wenyeji Spezia uongozini katika dakika ya 12 kabla ya Ivan Perisic kusawazishia Inter ya kocha Antonio Conte kunako dakika ya 39.

Awali, matumaini ya nambari mbili AC Milan kuwafikia Inter kileleni mwa jedwali la Serie A yalididimizwa zaidi na Sassuolo waliowapokeza kichapo cha 2-1 uwanjani San Siro.

Katika mchuano mwingine wa Jumatano usiku, Juventus walitoka nyuma na kuwacharaza Parma 3-1 katika ushindi ulioweka hai matumaini ya kikosi hicho cha kocha Andrea Pirlo kumaliza ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao wa 2021-22.

Mabao mawili kutoka kwa beki Alex Sandro yalisaidia Juventus kujinyanyua dhidi ya Parma waliofungiwa bao la mapema kupitia kwa Gaston Brugman kabla ya Matthijs de Ligt kusawazisha.

Baada ya mechi, kocha wa Sassuolo, Roberto de Zerbi, alifichua kwamba nusura ashawishike kukataa kusafiri na kikosi uwanjani San Siro kwa minajili ya mechi hiyo baada ya AC Milan kuwa miongoni mwa vikosi 12 vya kwanza kuingia katika kivumbi cha European Super League kilichopendekezwa kuanza Agosti 2021.

Mbali na AC Milan wanaotiwa makali na kocha Stefano Pioli, vikosi vingine vya Serie A vilivyohusishwa katika mpango wa kunogesha kivumbi cha ESL ni Inter Milan na Juventus.

Kabla ya kupulizwa kwa kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi kati ya AC Milan na Sassuolo, mkurugenzi wa AC Milan, Paolo Maldini, aliomba radhi kutoka kwa mashabiki kwa kuhusika kwake katika kuidhinisha ushiriki wa klabu hiyo kwenye kipute cha ESL ambacho kwa sasa kimesambaratika.

Atalanta ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini kwa alama 64, huenda wakapaa hadi nafasi ya pili jedwalini mnamo Aprili 22 iwapo watawakomoa AS Roma ugenini. AC Milan wanajivunia alama 66, moja pekee kuliko nambari tatu Juventus.

MATOKEO YA SERIE A (Aprili 21, 2021):

AC Milan 1-2 Sassuolo

Juventus 3-1 Parma

Spezia 1-1 Inter Milan

Bologna 1-1 Torino

Crotone 0-1 Sampdoria

Genoa 2-2 Benevento

Udinese 0-1 Cagliari

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Spurs watoka nyuma na kusajili ushindi wa 2-1 dhidi ya...

Barnaba Korir: Tuko tayari kuandaa Kip Keino Classic