Utata wazuka kuhusu BBI kaunti 34 zikipitisha mswada feki

Na WAANDISHI WETU

MCHAKATO wa BBI umo kwenye hatari ya kusambaratika baada ya kuibuka kuwa mabunge 34 ya kaunti yalipitisha mswada feki.

Taarifa zinaeleza kuwa kaunti hizo zilipitisha mswada uliokuwa na kipengee kilichokuwa na hitilafu kuhusu jinsi maeneo bunge mapya 70, yanayopendekezwa, yatakavyogawa.

Kutokana na dosari hiyo, Bunge la Kitaifa na Seneti zilipata nakala tofauti za Mswada wa BBI, hali ambayo imezua hali ya kuchanganyikiwa kwa wanachama wa kamati ya pamoja iliyokuwa ikiandaa ripoti ya mwisho, ambayo inatarajiwa kuwasilishwa mbele ya mabunge hayo mawili wiki ijayo.

Ni kaunti 13 pekee ambazo zilijadili na kupitisha nakala sahihi. Kaunti hizo ni Nyandarua, Nyeri, Murang’a, Embu, Nakuru, Tharaka Nithi, Meru, Mandera, Turkana, Laikipia na Siaya. Nayo Elgeyo Marakwet iliwasilisha nakala hizi mbili kwa pamoja.

Kufuatia hitilafu hiyo, wanaosukuma BBI sasa wameshikwa na hofu kuwa baadhi ya watu wakienda kortini kupinga mchakato huo kwa msingi kuwa nakala sahihi haikupitishwa na mabunge ya kaunti, wataweza kuzima shughuli hiyo.

Kinachoshangaza ni kuwa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliweka nakala sahihi kwenye tovuti, hivyo inazua maswali kule nakala yenye kasoro ilikotoka.

“Kutokana na kasoro hii, ni rahisi kwa mahakama kusimamisha shughuli hii,” akasema mwanachama wa kamati ya bunge.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alieleza kuwa walituma nakala walizopokea kutoka kwa watayarishaji wa mswada huo bila kufanyia mabadiliko yoyote.

Katibu mwenza wa ofisi kuu ya BBI, Paul Mwangi alisema haieleweki nakala ya pili yenye makossa ilikotoka.

Bw Mwangi alidai kuwa makosa hayo ni njama ya wapinzani wa BBI kuvuruga mchakato huo kupitia mahakama baada ya kushindwa kuuvuruga kisiasa.

Makosa hayo yaligunduliwa na wataalamu wawili wa sheria, Prof Patricia Mbote na Dkt Collins Mbote, ambao walikuwa wamepewa kazi ya kutoa ushauri kwa kamati ya pamoja ya bunge.

Habari zinazohusiana na hii

MAYATIMA WA BBI