• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
TAHARIRI: KNEC isiharakishe walimu na mtihani

TAHARIRI: KNEC isiharakishe walimu na mtihani

KITENGO CHA UHARIRI

TANGAZO la Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, kwamba matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) yatatolewa kufikia Mei 10, limeibua maswali kuhusu utaratibu utakaotumiwa kwenye usahihishaji wa mtihani huo.

Tayari, baadhi ya wadau wamekosoa mikakati iliyowekwa kwenye mchakato huo, wakisema unaharakishwa huku mazingira ya usahihishaji yakiwa si salama kwa baadhi ya walimu.

Katika hali hiyo, ni muhimu kwa waziri kutilia maanani baadhi ya hisia zinazotolewa na walimu, kwani ndio wahusika wakuu kwenye mchakato huo.

Vile vile, waziri anapaswa kufahamu kuwa la muhimu si kumaliza shughuli hiyo, bali kuhakikisha imeendeshwa kwa umakinifu mkubwa.

Haya yanatokana na baadhi ya malalamishi ambayo yametolewa kuhusu matokeo ya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE), ambapo baadhi ya shule za kibinafsi zimedai uwepo wa mapendeleo dhidi yazo ikilinganishwa na shule za umma.

Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo Anuwai (KUPPET) nacho kimeliomba Baraza la Kitaifa la Mitihani (KCSE) kutoendesha zoezi jijini Nairobi pekee kama ilivyo kawaida, ikizingatiwa eneo hilo ni miongoni mwa yale yaliyo na kiwango cha juu cha maambukizi ya virusi vya corona.

Kinaitaka KNEC kubuni vituo vya usahihishaji katika maeneo mengine nchini, ili kuwalinda walimu ambao miaka yao imesonga dhidi ya kuambukizwa virusi hivyo.

Chini ya masuala haya yote, ni wakati muhimu kwa Prof Magoha na maafisa wakuu katika Wizara ya Elimu kutilia maanani na kuzingatia malalamishi hayo.

Si vizuri kwa shughuli hiyo muhimu kuendeshwa katika hali ambapo baadhi ya walimu wanahisi kudhalilishwa ama kushinikizwa kwa namna fulani. Walimu pia wamekuwa wakilalamikia malipo duni kwa muda mrefu, ila hilo bado halijasuluhishwa.

Wito wetu kwa waziri ni kufahamu kuwa, ni muhimu kwa matakwa ya walimu kuzingatiwa kwani wanashiriki kwa zoezi ambalo linahusu mustakabali wa maelfu ya wanafunzi.

Itakuwa bora kwa shughuli hiyo kufanyika wakati kila upande unahisi kutotengwa wala kubaguliwa kwa namna yoyote.

Hilo litahakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora bila matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza awali.

You can share this post!

Utata wazuka kuhusu BBI kaunti 34 zikipitisha mswada feki

KAMAU: Wakenya tujiangalie upya jinsi tunavyoweka imani kwa...