• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KAMAU: Wakenya tujiangalie upya jinsi tunavyoweka imani kwa Mungu

KAMAU: Wakenya tujiangalie upya jinsi tunavyoweka imani kwa Mungu

Na WANDERI KAMAU

KWA mujibu wa takwimu kutoka kwa Sensa ya Kitaifa ya mwaka 2019, asilimia 80 ya Wakenya ni Wakristo huku asilimia 20 wakiwa Waislamu.

Takwimu hizi pia zinaonyesha kuwa mbali na makundi haya mawili, kuna Wakenya ambao wanafuata dini za Kihindi, Kiyahudi na kitamaduni. Wengine hawaanini kuhusu uwepo wa Mungu.

Hata hivyo, wale wasioamini uwepo wa Mungu ni kundi dogo sana, ambalo haliwezi kuwa na athari zozote kisiasa, kitamaduni wala kijamii.

Kiupana, Kenya ni taifa linaloongozwa kwa misingi ya Kikristo na Kiislamu.

Kwa mantiki hii, tarajio la kila mtu ni kuwa ikizingatiwa karibu asilimia 100 ya Wakenya wana utambulisho fulani wa kidini, basi tusingekuwa tukishuhudia maovu ambayo yanaendelea kujitokeza kila siku.

Tungekuwa nchi ya amani, taifa linaloongozwa na maadili, hali ya kujaliana na undugu.

Ikiwa tungekuwa tukizingatia udini huo, ingekuwa nadra kusikia matukio kama mauaji baina ya wapenzi au wanandoa, wizi wa mabavu, ubakaji au chuki miongoni mwa ndugu.

Kila siku ingekuwa ‘Siku Njema’ kwetu, kama alivyosema marehemu Prof Ken Walibora.

Tungekuwa tukiishi katika nchi mfano wa mbinguni; nchi isiyo na chuki wala wizi, ukabila wala ubaguzi, unyanyasaji wala mapendeleo.

Vyombo vya habari visingekuwa vikiripoti kuhusu ndugu waliouana kwenye mzozo wa urithi wa mali, au wapenzi waliouana kutokana na tofauti za kinyumbani.

Tusingekuwa tukisikia kuhusu wanafunzi wanaochoma shule kama ‘kisasi’ kwa walimu wao, wafanyakazi wanaogoma kwa kutolipwa mishahara yao au viongozi wanaofikishwa mahakamani kutokana na tuhuma za ufisadi.

Kenya ingekuwa kama mbinguni ya kidunia. Nchi ambako hekima ndiyo msingi mkuu wa kimaisha, ukabila usingekuwa chanzo cha migawanyiko na chuki za kisiasa huku ubaguzi ukikosa nafasi yoyote katika maisha yetu.

Hata hivyo, hali imekuwa kinyume. Licha ya udini wetu mkubwa, inasikitisha kwamba umwagikaji damu umegeuka kuwa sehemu ya maisha yetu. Hatujaliani hata kidogo!

Ubinadamu uliokuwepo nyakati za zamani haupo. Badala yake, mwanadamu amegeuka kuwa hayawani mkuu. Anamuua mwenzake kama mnyama kwa kosa dogo tu!

Ukabila uliokithiri katika idara mbalimbali za serikali umeifanya Kenya kuonekana kama inayomilikiwa na jamii moja pekee. Ukabila umegeuka kuwa wenzo mkuu unaozingatiwa kuamua ikiwa mtu fulani anafaa kuajiriwa katika idara fulani serikalini au la.

Maswali yanaibuka: Tunajidanganya kama jamii? Mbona maovu haya yanatokea katika nchi ambako nusura kila mtu anajitambulisha kuwa Mkristo, Muislamu, Mhindi ama Myahudi? Dini hizi ni za kweli ama ni mibandiko tu ya majina yasiyo na msingi wowote?

Binafsi, nahisi tunajidanganya. Tunamdanganya Mungu kwamba tu wana wake ilhali tunaendelea kufanya maovu kinyume cha mafundisho yake. Je, ni nini maana ya sala za kila Jumapili miongoni mwa Wakristo na kila Ijumaa miongoni mwa Waislamu ikiwa maovu, unyama na ukatili unaendelea kutuandama kila kuchao? Je, dini ina maana yoyote kweli katika jamii?

Bila shaka, umefika wakati ambapo tunafaa kutathmini mwelekeo wetu kama jamii ikiwa maovu haya yataendelea kutokea. Tathmini hii ni kuhusu nafasi ya dini katika maisha yetu.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: KNEC isiharakishe walimu na mtihani

KINYUA BIN KING’ORI: Ubaguzi na ukabila umekithiri...