• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
KINYUA BIN KING’ORI: Ubaguzi na ukabila umekithiri katika baadhi ya kaunti

KINYUA BIN KING’ORI: Ubaguzi na ukabila umekithiri katika baadhi ya kaunti

Na KINYUA BIN KING’ORI

SERIKALI nyingi za kaunti zimedhihirisha wazi kwamba zimejaa mapendeleo katika kuajiri wafanyakazi wa umma.

Upendeleo, ukabila na uonevu haukuwa mojawapo ya malengo ya wananchi kupendekeza kuongozwa na serikali za kaunti mashinani, magavana wakiwa viongozi wao.

Serikali hizi zinafaa kubadilsha mbinu zinazotumia kuajiri watumishi wa umma. Mbinu zinazotumiwa kwa sasa zimevunja moyo Wakenya wengi waliotarajia ugatuzi ungekuwa sindano au tiba ya kuponya maradhi ya ukabila, unyanyashaji, uonevu, kudharauliwa na upendeleo wakati wa kuajiriwa au kupata huduma muhimu kutoka kwa serikali.

Namna wanavyoajiriwa watumishi wa umma inazua maswali mengi na imethibitika kuwa hakuna kanuni zinazozingatiwa ila ubaguzi mtupu. Hata, baadhi ya magavana wamezoea kuteua makatibu wa kaunti na wafanyakazi wengine kutokana na kujuana au urafiki badala ya uzoevu na elimu ya mhusika.

Kwa mfano, katika kaunti mojawapo Pwani, watu wa familia moja wameajiriwa kushikilia nyadhifa mbalimbali. Sikwambii katika baadhi ya ofisi ambapo watu wanaotekeleza majukumu mbalimbali wengi wametoka kwenye ukoo mmoja huku wakazi wengine wakibakia bila kazi licha ya kuwa wenye elimu, ujuzi na tajriba.

Naelewa haiwezekani kila mmoja kupata ajira katika serikali, ila itakuwa kosa kazi hizo kutumika kama chambo kisiasa. Kwa nini watu waajiriwe kwa msingi wa ukoo anaotoka kiongozi fulani? Ubaguzi wa kiukoo sasa umekuwa maradhi yanayopasua azma ya ugatuzi mashinani.

Hali hii ndiyo imefanya baadhi ya wananchi wa kawaida kukosa kuonea fahari ugatuzi mashinani kiasi cha wengine kuanza kutamani kurejeshwa kwa mfumo wa zamani wa Serikali Kuu na kufutiliwa mbali kwa utaratibu wa utawala wa kaunti.

Wakenya waliojitolea kupambana ili katiba ya zamani ifanyiwe mageuzi yaliyozaa ugatuzi, walikuwa wamesinywa na mfumo huo uliokuwa ukipendelea baadhi ya watu katika ajira, ugavi wa mapato ya kitaifa na ubaguzi katika maamuzi muhimu yanayogusa maisha yao.

Shughuli zote muhimu zilizogatuliwa zinafaa kuendeshwa kwa njia ya uwajibikaji, uwazi na haki kuchangia kuimarisha uchumi wa kaunti na maendeleo. Kuajiri watu kwa msingi wa upendeleo au kufuta wengine kwa uonevu wa kisiasa ni jambo linalopaswa kukomeshwa ili ugatuzi uwe wenye manufaa kwa wananchi.

Magavana wanafaa kuwa mfano bora kwa kukoma kufanya mambo yanayokwaza ugatuzi kiasi cha raia kuonekana kukosa imani na serikali za ugatuzi kutokana na jinsi wanavyotekeleza majukumu yao.

You can share this post!

KAMAU: Wakenya tujiangalie upya jinsi tunavyoweka imani kwa...

AKILIMALI: Ufugaji samaki kwa madema waleta kipato