• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
AKILIMALI: Usanii wake wa kutumia penseli umemjengea jina

AKILIMALI: Usanii wake wa kutumia penseli umemjengea jina

Na SAMMY WAWERU

PAXSON Mambo, mwenye umri wa miaka 20, anaendelea kupalilia kipaji chake katika uchoraji na ambacho kinampatia kila sababu ya kutabasamu.

Uchoraji ndio kazi yake ya kila siku, huiamkia kila asubuhi na kabla ya siku kuisha anahakikisha ameafikia malengo yake.

Hakutambua amejaaliwa talanta ya uchoraji leo, jana wala juzi.

“Nikiwa mdogo kiumri nilivutiwa sana na michoro kwenye mabango na matatu na eneo lolote lile lenye michoro,” anadokeza.

Kulingana na Paxson maarufu kama Pakii Mchoraji, kila angepelekwa jijini au maeneo ya mijini alikuwa akishawishi mzazi aliyeandamana naye akague michoro kwa kina.

Isitoshe, alipenda kuabiri matatu yenye michoro hasa ya wasanii.

Anakumbuka kana kwamba ilikuwa jana tu akiwa shuleni si mara moja, mbili au tatu alikuwa akizozana na walimu kwa sababu ya mazoea yake kugeuza madaftari na pia vitabu vya kusoma kuwa ‘uga’ wa michoro.

“Dawati langu na ya wanafunzi marafiki yalijaa michoro,” Paxson asema.

“Ni hatua ambayo ilimshawishi baba kunipeleka jijini Nairobi mara kwa mara na kuhakikisha tunaingia kila eneo lenye michoro na michongo,” aelezea.

Ilikuwa fursa ya kipekee na iliyomwezesha kutazama michongo ya baadhi ya mashujaa waliopigania uhuru wa Kenya na demokrasia, kama vile Dedan Kimathi na Tom Mboya.

“Nilikuwa ninachora upya sura nilizotama, kupitia usaidizi wa picha kwenye vitabu,” anasema.

Paxson anasema baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE 2018 alichora picha ya mwanasoka tajika Cristiano Ronaldo, anayechezea Klabu ya Juventus kwa sasa, picha ambayo ilmridhisha mama yake.

Aidha, aliichora kwa kalamu ya mate, penseli.

“Ilimfurahisha kiasi cha kuniomba nichore picha ya babu, akainunua Sh200 akampelekea kama zawadi,” anafichua msanii huyo mchanga.

Alipakia mitandaoni kwa Facebook na Instagram, picha hizo, na kwa mujibu wa masimulizi yake hivyo ndivyo aligeuza talanta yake kuwa uchoraji-biashara.

“Nilipata oda kadha za wachangiaji mitandao. Mteja wa kwanza alitaka nimchore picha yake, tukaafikiana malipo ya Sh700 japo alinilipa Sh150 pekee.

“Yalikuwa kiduchu, lakini sikukadiria hasara kwa sababu nilitumia penseli ya Sh10 na karatasi ya manila ya Sh5 pekee,” Paxson anafafanua.

Aidha, alichora picha za mastaa maarufu katika ulingo wa muziki kama vile King Kaka, Nadia Mukami, Miracle Baby, kati ya wengineo, michoro ambayo ilimvunia sifa.

Katika chumba chake, ingawa cha kukodi kilichoko mtaa maarufu wa Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi, na ambacho pia ni karakana yake tunampata akishughulikia oda kadhaa.

“Wachoraji wengi hutumia rangi maalum (acrylic), ila mimi hutumia penseli au kalamu ya wino,” asema. Ni hatua ambayo inaufanya ubunifu wa Paxson kuwa wa kipekee.

Mbali na vifaa anavyotumia kuchorea, vifaa vingine anavyotumia ni pamoja na karatasi ya manila, brashi ya kupodoa, kifutio, wembe na shashi.

Huanza kwa kupokea picha ya mteja, anaikagua kwa umakinifu, simu ikiwa kiungo muhimu katika shughuli za kuchora.

“Hutumia simu ya kisasa kuhariri picha, iwe rangi anayotaka mteja na itakayoniongoza. Ni mfumo wa teknolojia ambao umenisaidia kuimarisha maarifa katika kuchora,” anaelezea barobaro huyo, akionyesha hatua anazofuata, kuanzia kuwa na muongozo wa mchoro hadi kupata picha halisi.

Picha inapokamilika, pia huiweka kwenye fremu, ya hivi punde kuchora ikiwa ya msanii wa kibao cha Firirida uliotungwa na mwanamuziki wa nyimbo za lugha ya Kikuyu, Dick Munyonyi zaidi ya miaka 32 iliyopita.

Mwaka wa 1989, Mzee Munyonyi alitumbuiza katika harusi ya Rais wa sasa Uhuru Kenyatta, na kulingana na Paxson picha yake aliyoichora kwa penseli inaendelea kusambaa mitandaoni na kumvutia ofa.

Mwanasanaa huyu huchora picha ya mtu binafsi, familia, maadhimisho ya hafla, wasanii na wanasiasa, kati ya wengineo, huku malipo yake yakiwa kati ya Sh1, 500 – Sh9, 500.

Kwa siku huchora picha mbili au tatu, kiwango cha mauzo kikitegemea oda anazopata.

“Hutoza bei kulingana na saizi ya picha, yaliyomo, idadi ya watu na aina ya fremu,” asema.

Huku nembo yake ikiwa Pakii Mchoraji, mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Instagram imemfaa pakubwa kupata wateja.

Sawa na wasanii wengine, Paxson anasema kikwazo kikuu ni ukosefu wa fedha za kutosha kuboresha jitihada zake.

“Sekta ya usanii inahitaji kupigwa jeki na serikali, ina vipaji wengi waliojaaliwa talanta. Walichokosa ni hamasisho na fedha kujiimarisha,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano, akihimiza asasi husika kutathmini mikakati ya kuwatambua na kuwainua.

“Wasanii wa michoro na michongo wakiinuliwa watakuwa na mchango mkubwa katika kuangazia suala la ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana. Changamoto zinazowakumba, ni kukosa hamasa na jukwaa la kujiimarisha. Wengi wao huishia kufa moyo,” anaeleza Joseph Njoroge, mchoraji tajika eneo la Ruiru.

Wakiimarika, ina maana kuwa serikali itakuwa imeongeza viteka vingine kukusanya kodi na ushuru.

Licha ya pandashuka zinazomzingira Paxson Mambo, anasema ni kwa muda tu jina lake liwe la kupigiwa upatu nchini na katika kiwango cha kimataifa sawa na kielelezo wake, Joseph Njoroge ambaye jitihada zake zimeangaziwa na vyombo vya habari vya

You can share this post!

AKILIMALI: Anakula jasho lake kwa kilimo cha mkunde na...

KCSE: Matokeo kutolewa Mei