• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
KCSE: Matokeo kutolewa Mei

KCSE: Matokeo kutolewa Mei

Na WANDERI KAMAU

WATAHINIWA wa Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka huu watajua matokeo yao kufikia Mei 10, amesema Waziri wa Elimu, George Magoha.

Akihutubu jana katika Shule ya Upili ya Nairobi School, jijini Nairobi, Prof Magoha alitangaza mtihani huo uliendelea vizuri bila matatizo yoyote kama ilivyoratibiwa.

Aliwasifia watahiniwa wote 752,891 kwa kuonyesha ukakamavu mkubwa, kwani walifanya mtihani huo katika mazingira magumu kutokana na janga la virusi vya corona.

“Mmefanya mtihani huu katika nyakati ngumu sana, ambapo mwanzoni, ilikuwa hata vigumu kwetu kuelewa ikiwa zoezi hilo lingefaulu kutokana na hali ilivyo nchini kutokana na janga hili. Hata hivyo, nawashukuru wadau wote waliohusika kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa,” akasema waziri.

Kuhusu njama za wizi wa mitihani, alisema walifanikiwa kuzima mipango yote iliyokuwa imepangwa kutekeleza uovu huo katika vituo vichache nchini.

“Tulikumbana na visa kadhaa ambapo baadhi ya maafisa waliosimamia mitihani hiyo walijaribu kuifungua kabla ya muda ufaao. Tulifanikiwa kuzima visa hivyo kwenye vituo vichache vilikoripotiwa,” akasema.

Kutokana na visa hivyo, maafisa 27 wa kusimamia mitihani walipokonywa majukumu hayo.

Majina yao yanatarajiwa kuwasilishwa kwa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) ili kuchukuliwa hatua za kinidhamu na Wizara ya Elimu.

Wakati wa mtihani huo, watu 37, wakiwemo wanafunzi watatu wa vyuo vikuu walikamatwa kwa kujaribu kufanya wizi wa mitihani hiyo.

Kando na hayo, simu 53 za rununu zilitwaliwa kutoka kwa wanafunzi katika sehemu mbalimbali nchini.

“Kwa sasa, vikosi vya usalama vinaendesha uchunguzi kubaini ikiwa simu hizo zilitumika kwa namna yoyote ile kutekeleza wizi,” akasema.

You can share this post!

AKILIMALI: Usanii wake wa kutumia penseli umemjengea jina

NASAHA ZA RAMADHAN: Kusaidia masikini kusiwe tu wakati wa...