• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
MATHEKA: Uraibu wa Jubilee kukaidi maagizo ya korti ni aibu kubwa!

MATHEKA: Uraibu wa Jubilee kukaidi maagizo ya korti ni aibu kubwa!

Na BENSON MATHEKA

UAMUZI wa Mahakama Kuu kwamba mawaziri wanane waliohudumu muhula wa kwanza wa serikali ya Jubilee na mawaziri wote wasaidizi wako ofisini kinyume cha sheria unadhihirisha kiwango cha upuuzaji wa Katiba na watu waliotwikwa jukumu la kuilinda, kuitetea na kuiheshimu.

Si ajabu uamuzi huo ukapuuzwa na badala yake, mahakama ikalaumiwa kwa kuhujumu serikali. Hali kama hii hufanyika mara nyingi nchini na imekuwa kama kawaida. Viongozi wakuu wa serikali wameonyesha mfano mbaya wa kuchochea umma dhidi ya Mahakama huku wakitetea makosa yao. Wamekuwa wakipaka matope mahakama ili ionekane kama ndiyo kizingiti kwa utekelezaji wa maendeleo.

Wamefanikiwa kufanya hivi kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kukataa kuapisha majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Mahakama (JSC) katika juhudi za kuongeza kasi ya utoaji wa haki. Licha ya kukataa kuapisha majaji hao, viongozi wa serikali wamekuwa katika mstari wa mbele kukosoa mahakama kwa kucheleweshwa kesi.

Lengo la maafisa wa serikali ni kuwa na Mahakama dhaifu ambayo wataielekeza watakavyo katika juhudi zao za kukandamiza raia. Hawataki yeyote anayetetea maslahi ya umma. Hawataki yeyote anayetetea haki za kina yakhe. Hii ndio sababu wamekuwa wakipiga vita wanaharakati wanaoenda kortini kupinga maamuzi ya serikali wakidai wanawahonga majaji wawapendelee katika maamuzi yao. Wanachotaka, na ambacho wamefaulu kwa kiwango fulani, ni kuzima mahakama ili isifanye maamuzi ya haki kama kuharamisha nyadhifa za manaibu wa mawaziri ambazo haziko katika Katiba.

Uhalalishaji

Pengine hii ndiyo sababu wanataka kubadilisha Katiba ili kuhalalisha makosa yao. Liwe liwalo, ukweli utadumu kwamba serikali ya Jubilee imekuwa ikikaidi Mahakama, ikitelekeza utawala wa sheria na kutumia njia za mkato ambazo zikikosa kurekebishwa, zitatumbukiza nchi hii kwenye mzozo mkubwa.

Kwa serikali ya Jubilee, kuheshimu Katiba imekuwa hiari ilhali haifai kamwe kuwa hiari, kila Mkenya anafaa kuheshimu Katiba.

Waliokula kiapo cha kuilinda na kuitetea Katiba wanapokuwa wa kwanza kuikaidi, huwa kuna hatari kubwa na wanaoumia ni akina yakhe. Hatari hii inajitokeza kwa kuzima na kutisha wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu.

Uraibu wa serikali ya Jubilee wa kukaidi maagizo ya Mahakama, utaua demokrasia na uchumi wa nchi. Itakumbuka kwamba tabia kama hii imewahi kuwa katika mataifa mengine ikiwemo Kenya wakati wa utawala wa chama cha Kanu. Ukiukaji Katiba unafaa kulaaniwa na kila mmoja wetu.

You can share this post!

Madai ya hujuma huku BBI ikibadilishwa kisiri

OMAUYA: Mikopo inaalika utumwa na zigo la deni kwa vizazi...