• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
OMAUYA: Mikopo inaalika utumwa na zigo la deni kwa vizazi vijavyo

OMAUYA: Mikopo inaalika utumwa na zigo la deni kwa vizazi vijavyo

Na MAUYA OMAUYA

KUNA neno wanalosema wazee wa mambo kuhusu chupi ya kuazima.

Sitarudia stori yote ya chupi hapa lakini nitafananisha hali ya nchi ya Kenya na chupi ya kuazima; ni balaa tupu na tusi kwa mababu waliopigania uhuru, ni kero kwetu sisi tunaobeba zigo hilo na ni laana kwa vizazi vijavyo.

Rais Uhuru Kenyatta atasalia kwenye kumbukumbu kama Rais aliyezima mwanga wa kujitegemea na kututia kwenye giza la maangamizi kupitia kwa matrilioni ya deni.

Miongo saba baada ya kujitwalia uhuru, ni aibu kwa raia wa Kenya kuona kwamba taifa lao sasa liko kwenye lindi la msiba wa deni. Hakuna nchi inayoweza kustawi iwapo uzalishaji wake mwingi unaelekezwa katika kulipa madeni ambayo serikali imebugia kama mvinyo. Inavunja moyo zaidi kuona kwamba kiwango cha mkopo na mapato kwa jumla huishia katika domo lisiloshiba la ufisadi na ufyonzaji.

Elimu ya Siasa na Uchumi haikatai nchi kuomba mkopo kwa wastani kupitia utaratibu ufaao. Ukweli ni kwamba kila taifa lililostawi limekopa, hata Marekani na ukwasi wake wana mkopo. Ukitazama Ulaya baada ya 1945, mataifa mengi yaliwezeshwa kupitia mpango wa Marshall Plan. Mataifa kama Italia, Ugiriki na Uhispania yanaendelea kujikimu kupitia mikopo ya EU na Ujerumani.

Wakati mwingi mikopo ya aina hii huwa na dhamira moja tu, kuziba pengo kwenye bajeti ya nchi au kuzuia taifa kuzama na kuhatarisha usalama wa raia. Mataifa mengine pia hupata mikopo kama njia ya kujisitiri kufuatia dharura fulani. Haya yanaeleweka! Lisiloeleweka ni pupa ya Kenya katika kujilimbikizia madeni. Ninamlenga mno Uhuru Kenyatta kwa sababu amewahi kuwa waziri wa fedha na anaelewa barabara kwamba mikopo isiyokuwa na dari inalipatia taifa raha ya muda kisha karaha ya daima!

Uchumi

Uhuru ni mtu aliyebobea kwa maarifa kuhusu uchumi wa nchi na angefaa kuelekeza taifa hili kwenye bandari salama kiuchumi. Balaa ni kwamba atakapoondoka ikulu mwaka ujao, Kenya itakuwa kwenye kikaango cha China, IMF, Wold Bank na wafadhili wengine. Kila anaponadi miradi ya maendeleo ya miundo msingi kama vile SGR, Uhuru yafaa akumbuke msemo ule ule wa ‘chupi ya Kuazima…” Kuna kukopa na kuna kuzama mikoponi!

Ni aibu kubwa kwa nchi kusema tumejipa reli ya kisasa na mabarabara ya kuvutia iwapo tutatumia watoto ambao hawajazaliwa kulipa deni letu. Ndio maana Rais Uhuru angefaa kutopuuza hasira ya hivi majuzi ambapo Wakenya mitandaoni walikabili IMF na kutaka chirika hilo lisipatie Kenya mkopo. Hatua ilionekana ya kipuuzi tu lakini inaashiria kero walio nao raia wa nchi hii.

Waswahili husema anayehitaji hana haya lakini katika hali ya sasa ya Kenya, imefikia kiwango watoto wanamwambia jirani “Usimkopeshe Dadi, hatuhitaji!, kisha anatudhulumu” Hii ni kwa sababu kosa kubwa la Uhuru Kenyatta sio kukopa kupita kiasi tu. Kosa linalokeketa maini zaidi ni kukiri kwamba anajua taifa hili ‘linalokopa’ linapoteza angaa bilioni mbili kila siku kupitia ufisadi. Baada ya kukiri haya, ikumbukwe aliwahi kusema hadharani “Mnataka nifanye nini jamani?”

TF Body text: Deni hunyima taifa lolote uhuru wa kweli. Kwa kutegemea deni, taifa hujiingiza minyororo ya utumwa. Baada ya kubugia deni, itafika siku itabidi tutoe raslimali zetu muhimu kwa wafadhili waendeshe. Itakuwa msiba wa kihistoria iwapo China itafikia kuendesha bandari na viwanja vya ndege humu nchini kwa sababu deni limezidi kiwango. Laana iliyoje? Tusipoziba ufa kwa kuasi tamaa ya mikopo, tutajenga ukuta kwa kukabiliana na utumwa baadaye.

[email protected]

You can share this post!

MATHEKA: Uraibu wa Jubilee kukaidi maagizo ya korti ni aibu...

TAHARIRI: Jaji Mkuu hatamaliza shida za mahakama