• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
TAHARIRI: Jaji Mkuu hatamaliza shida za mahakama

TAHARIRI: Jaji Mkuu hatamaliza shida za mahakama

KITENGO CHA UHARIRI

TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) leo inakamilisha kumhoji mtu wa kumi katika mchakato wa kumsaka mrithi wa Jaji Mkuu, David Maraga.

BVaada ya kumhoji Bi Alice Yano, kibarua kitakuwa kusubiri uamuzi wa mahakama kuhusu uamuzi uliotolewa Jumatano na majaji watatu. Majaji Anthony Mrima, Wilfrida Okwany na Richard Nyakundi walisimamisha kwa muda JSC kuendelea na mahojiano ya kumsaka Jaji wa Mahakama ya Juu.

Mahojiano yanayoendelea ni ya kujaza nafasi ya Jaji Mkuu, na ilikuwa imepangwa kwamba kuanzia Jumatatu JSC ingeanza kuwahoji wanaotaka kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu, nafasi iliyoachwa na Prof Jackton Ojwang.

Walisema masuala yaliyowasilishwa mbele yao katika kesi nne tofauti ni mazito, na hayawezi kupuuzwa.

Kutokana na uamuzi huo wa Jumatano, JSC ikikamilisha mahojiano ya leo, haitaruhusiwa kujadiliana na kuteua jina litakalowasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Wakati tume hiyo ikisubiri kujua hatima ya rufaa yake, inapaswa kuchukua muda kuyaangazia baadhi ya masuala yaliyojitokeza kwenye mahojiano kwa wiki mbili zilizopita. Suala moja kuu ni mrundiko wa kesi katika mahakama.

Majaji wote, akiwemo Rais wa Mahakama ya Rufaa, Bw William Ouko walikiri kuwepo kwa mrundiko wa kesi. Kwa sasa kuna mrundiko wa zaidi ya kesi milioni moja ambazo hazijaamuliwa.

Baadhi ya kesi hizo zimekaa kwa zaidi ya miaka 15, huku baadhi ya waliotafuta haki wakiwa wameshafariki dunia.

Tatizo jingine linalohitaji kuangaziwa ni sifa ya idara ya mahakama kuhusiana na ufisadi. Maelfu ya Wakenya wanaamini kwamba ili kupata haki, ni lazima mlalamishi atoe kitu kidogo kwa majaji, mahakimu, makarani wa korti au watumishi wengine wa mahakama.

Sifa hiyo mbaya itachukua muda mrefu kuondoka. Ingawa inachukuliwa kuwa dhana, mamia ya wananchi waliopoteza kesi dhidi ya watu wenye usemi wa kifedha, watasema ushindi hupewa wenye nguvu.

Kila aliyehojiwa alitakiwa aeleze atakachofanya akiwa Jaji Mkuu. Swali hilo halionekani kuwa la msingi kwa sababu mrundiko wa kesi na ufisadi ni tatizo la idara nzima ya mahakama. Litatuliwe sasa, badala ya kumsubiri Jaji Mkuu mpya.

You can share this post!

OMAUYA: Mikopo inaalika utumwa na zigo la deni kwa vizazi...

NASAHA ZA RAMADHAN: Kila mmoja ajihadhari wakati wa ibada