• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
MKU yashirikiana na KFS kutekeleza miradi ya upanzi wa miti

MKU yashirikiana na KFS kutekeleza miradi ya upanzi wa miti

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) na Shirika la Kuhifadhi Misitu Nchini (KFS) zinashirikiana kutekeleza miradi ya upanzi wa miti kila mwaka.

Mnamo Alhamisi pande zote mbili ziliungana kwa upanzi wa miti 3,000 mjini Thika na kuhudhuriwa na mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho Prof Simon Gicharu na wakuu kadha wa KFS.

Prof Gicharu alisema chuo hicho litakuwa mstari wa mbele kushiriki upanzi wa miti kwa minajili ya kuendeleza uhifadhi wa miti kila mwaka.

“Tunashirikiana na serikali kwa kuhifadhi mazingira tukiangazia ruwaza ya 2030,” alisema Prof Gicharu.

Prof Gicharu, ambaye alishiriki katika hafla hiyo alitaja mwongozo wa ‘Panda miti, penda Kenya’ huku pia akitaja Chuo Kikuu cha Norttingham Trent University (NTU), na washirika wengine.

Walipokea ufadhili wa Sh850,000 kutumika kuhifadhi msitu wa Brakenhurst ulioko mjini Limuru. Alisema msitu huo una umuhimu wake kwani dawa za mimea zinatoka katika eneo hilo. Kulingana na mikakati hiyo eneo hilo linastahili kuhifadhiwa vilivyo ili kuzuia uharibifu kutoka nje.

Dkt Jared Onyancha ambaye aliongoza hafla hiyo alisema mwelekeo huo wa kuhifadhi misitu utadumishwa kwa minajili ya kuhifadhi mazingira kwa siku zijazo.

“Leo ni siku muhimu kwetu kwani tutazidi kushirikiana na KFS ili tuhifadhi mazingira jinsi inavyofaa. MKU pia itakuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba kila mwaka inashiriki upanzi wa miti,” alisema Dkt Onyancha, na kuongeza wanafunzi pia watapata nafasi ya kufanya utafiti wao huko.

Bw James Mwang’ombe ambaye alikuwa mgeni wa heshima katika hafla hiyo alisema uhifadhi wa mazingira utazingatiwa kila mara kwa ushirikianao wa pande zote mbili.

“Tunastahili kuhifadhi miti kwa wingi ili tuweze kupata dawa kutoka kwa misitu, kwa manufaa ya binadamu na wanyama,” alisema Bw Mwang’ombe.

Alipongeza MKU kwa kuhifadhi eneo maalum – Botanic Garden – la kuhifadhi miti huku akisema watazidi kuwapa usaidizi wakati wowote wakihitaji.

Naibu Chansela wa MKU Prof Deogratius Jaganyi, alisema ushirikiano wa shule na vyuo pamoja na KFS utaendelea kutekeleza upanzi wa miti wa kila mara ili kuafikia malengo ya serikali kupata asilimia 10 ya upanzi wa miti ifikapo mwaka 2030.

Dkt Vincent Gaitho wa MKU alisema eneo lililotengwa la Botanic Garden mjini Thika ni muhimu hasa kwa chuo hicho kwa sababu litakuwa mahali pa kufanya utafiti kwa masomo ya sayansi hasa kemia, biolojia, kilimo, mazingira na maswala ya mimea.

“Wanafunzi wengi watakuwa mstari wa mbele kunufaika na utafiti watakapokuwa wakijiendeleza katika eneo hilo. Kwa hivyo chuo chetu kitanufaika pakubwa,” alifafanua Dkt Gaitho.

You can share this post!

Napoli walima Lazio 5-2 huku Atalanta wakitoshana nguvu na...

Kuhimiza mawasiliano ya pande nyingi na kushirikiana...