BBI mikononi mwa wabunge

Na BENSON MATHEKA

MSWADA wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), sasa uko katika mikono ya maseneta na wabunge baada ya kamati ya pamoja inayoshughulikia mswada huo kuupitisha.

Kamati hiyo ilisema ilipitisha mswada huo hata baada ya kubaini kwamba, mabunge 32 ya kaunti yalijadili na kupitisha mswada uliokuwa na makosa.

Kupitishwa kwa mswada huo baada ya madai kuibuka kwamba kulikuwa na njama ya kuubadilisha au kuulemaza, ni hatua kubwa kuelekea kura ya maamuzi ya kubadilisha katiba ya 2010.

Hata hivyo, mjadala katika vikao vya bunge unatarajiwa kuwa mkali hasa kutoka kwa washirika wa Naibu Rais William Ruto ambao hawajaukumbatia.

Washirika wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ambaye ni kinara mwenza wa handisheki iliyozaa mchakato huo walikuwa wamedai kwamba, kulikuwa na njama ya kubadilisha mswada huo.

“Nataka kusema hivi, maadui wa BBI na wa handisheki wamepata washirika katika kamati ya pamoja ya bunge ya masuala ya sheria kuyumbisha mchakato wa BBI,” mbunge wa Ugunja Opiyo Wandari alinukuliwa akisema mapema wiki hii.

Hii ilijiri baada ya kuibuka kuwa, baadhi ya mswada huo ulikuwa na dosari.

Baadhi ya wanachama walikuwa wamedai kwamba, bunge inajukumu la kutekeleza katika mchakato wa kubadilisha katiba kwa kufanyia marekebisho mswada huku wengine wakipinga.

Ilibidi kamati kutafuta maoni ya wataalamu wa katiba walioshauri kwamba baada ya kupitishwa na mabunge ya kaunti, mswada huo hauwezi kubadilishwa.

Kulingana na kamati hiyo, makosa iliyopata kwenye mswada uliopitishwa na mabunge 32 ya kaunti ni madogo na yanaweza kurekebishwa.

Kwenye ripoti iliyopitishwa kujadiliwa kwenye vikao vya wabunge na maseneta, wenyekiti wa pamoja wa kamati iliyoshughulikia mswada huo, Seneta Okong’o Omogeni wa Nyamira na mbunge wa Kangema Muturi Kigano walisema kwamba, kamati iligundua makosa katika miswada iliyopitishwa na mabunge 32 ya kaunti.

“Tumegundua makosa ambayo yanaathiri kaunti 32 na hayo tumenakili katika ripoti yetu ambayo tumewasilisha ijadiliwe na vikao vya bunge na seneti,” Bw Omogeni aliambia wanahabari.

Mabunge 43 yalipitisha mswada wa BBI na kwa mujibu wa ripoti ya kamati, ni mabunge 11 yaliyopitisha mswada ambao haukuwa na makosa.

Bw Kigano amesema kwamba, baada ya kujadiliwa na seneti na bunge la kitaifa, mswada huo utapigwa msasa na Mwanasheria Mkuu kabla ya kuwasilishwa kwa kura maamuzi.

Wanachama wote wa kamati ya pamoja ya seneti na bunge la taifa, walitia saini ripoti hiyo isipokuwa seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata.

Bw Kang’ata alikanusha madai ya wenzake kwamba, alipinga mswada huo akisema umekuwa ukiendeshwa kwa siri na una dosari ambazo zingepigwa msasa kama mchakato mzima ungeendeshwa kwa uwazi.

Mnamo Alhamisi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikanusha kwamba iliwasilisha miswada miwili tofauti kwa mabunge ya kaunti mmoja ukiwa na dosari.

Kwenye taarifa, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema mswada waliowasilisha kwa mabunge yote ya kaunti ni uliochapishwa na kamati simamizi ya BBI.

“Tume ingetaka kueleza kwamba mnamo Disemba 10, 2020, ilipokea nakala sita zilizochapishwa za mswada wa BBI kutoka kwa waandalizi wa mswada wa marekebisho ya katiba wa 2020 na maelezo ya waliouunga mkono,” alisema Chebukati.

Baada ya kukagua saini na kuthibitisha uliungwa na wapigakura wasiopungua 1 milioni, tume iliitisha nakala zaidi ambazo ilituma kwa mabunge ya kaunti.

Habari zinazohusiana na hii

MAYATIMA WA BBI