• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
FATAKI: Uwongo wa waume ni mwingi; ni jukumu lako kuujua na kujiondoa

FATAKI: Uwongo wa waume ni mwingi; ni jukumu lako kuujua na kujiondoa

Na PAULINE ONGAJI

SUALA la migogoro ya kimapenzi baina ya wanawake na wanaume ambao ni waume wa watu sio geni.

Limekuwepo tokea zamani.

Mara nyingi mahusiano haya huisha vibaya, ambapo mara nyingi ni mabinti huishia kuumia.

Kwa mfano, siku kadhaa zilizopita binti mmoja alinisimulia kisa cha kaka fulani – mume wa mtu – aliyemhadaa kwa miaka mingi, huku akimdanganya kwamba angemuoa. Kaka huyo alipoamua kushika njia, binti huyo aliachwa na machungu ya kutemwa.

Mara nyingi najua kwamba ni wanaume wanaopaswa kulaumiwa kwa kuwanasa mabinti mtegoni, ilhali wanafahamu kwamba wameoa, ukweli ni kwamba vidokezi kuhusu ndoa zao huwa wazi hasa kupitia uwongo wanaosema.

Kwa mfano, “nitamuacha mke wangu na kukuoa kwani simpendi”. Mabinti wengi wamepoteza wakati wao wakimsubiri kaka atimize ahadi hii ambayo mara nyingi haitimii.

Nakumbuka kaka mmoja alinisimulia jinsi alivyokuwa akimtafuna binti mmoja huku akimhadaa kwamba angemuoa. Kaka huyu ana mke na japo alikiri kufurahia uhondo, alisema wazi wazi kwamba uhusiano wao ni wa muda tu, na kamwe hanuii kumuacha mkewe.

Nakubali kwamba kunao madume ambao hatimaye huwaacha wake wao na kuwaendea vimada, lakini hiyo ni asilimia ndogo sana, na pia kwangu ni dharau kwa mtu kukushawishi ukae pembeni ukisubiri amuache mkewe. Hii ni sawa na paka au mbwa anayekaa chini ya meza akitumai kwamba atarushiwa makombo kutoka mezani.

Udanganyifu mwingine ni kwamba “mke wangu hajui burudani”. Uongo huu hutumiwa kuwalaghai mabinti kudhani kwamba wana thamani, ambapo huu ni utapeli unaotumiwa na madume kama mbinu ya kuendelea kupokea uhondo pasipo gharama zozote.

Kisha kuna “natamani ningekutana nawe miaka kadha iliyopita”, au “hatulali kwenye kitanda kimoja,” uwongo ambao nia yake ni kumshawishi binti akubali nafasi ya pili, au aridhike na kuwa kitafunio cha pembeni, pasipo kutaka zaidi kutoka kwa dume husika. Pia, huenda umesikia huu uwongo. “Tuko pamoja kwa sababu ya watoto.” Udanganyifu huu pia unanuiwa kumfanya binti aridhike na nafasi ya pili bila maswali.

Kumbuka kwamba ni wajibu wako kulinda hisia zako, na hivyo ni jukumu lako kutambua hawa waongo na kutoweka, kabla uachwe ukilia.

[email protected]

You can share this post!

CHOCHEO: Usimpe mpenzi wako sababu ya kukushuku

MWANAMUME KAMILI: Mume kamili hawezi kumtoa uhai mkewe