• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Ombi Oparanya, Joho waachie Raila urais 2022

Ombi Oparanya, Joho waachie Raila urais 2022

Na IAN BYRON

KUNDI la wabunge wa ODM limemtaka Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho kuunga mkono kinara wao Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Viongozi hao wakiongozwa na Mwakilishi wa Wanawake wa Migori Pamella Odhiambo na mbunge wa Nyatike Tom Odege, jana walisema kuwa Bw Odinga atawania urais mwaka ujao na hataunga mkono mwaniaji yeyote.

Bw Oparanya na Bw Joho tayari wametuma maombi ya kutaka kuwania urais kupitia tiketi ya chama cha ODM. Lakini Dkt Odhiambo na Bw Odege wamewataka kujiandaa kumenyana vikali na Bw Odinga katika kura za mchujo.

“Kiongozi wetu wa chama atawania urais 2022 na mwanasiasa yeyote asitarajie kuidhinishwa. Bw Odinga amepigania mabadiliko mengi nchini hivyo anafaa kupewa fursa ya kuongoza nchi,” Dkt Odhiambo akaambia Taifa Leo.

Kulingana na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Bw Odinga hakuwa miongoni mwa waliotuma maombi ya kutaka kuwania urais kupitia tiketi ya ODM kufikia Machi 31, 2021 – ambayo ilikuwa siku ya mwisho kuwasilisha maombi.

Bw Odinga, hata hivyo, yuko huru kuwasilisha ombi lake wakati wowote kwa sababu hakuna kizuizi cha sheria, kulingana na mwenyekiti wa ODM John Mbadi.

Bw Odege alisema kuwa Bw Odinga amejitolea mhanga kupigania nchi hivyo anastahili kupewa heshima ya kuongoza taifa hili.

Mbunge wa Nyatike alisema kuwa Bw Odinga ana tajriba ya juu katika masuala ya uongozi ikilinganishwa na wanasiasa wengine ambao wametangaza azma ya kuwania urais mwaka 2022.

Chama cha ODM kilitoa notisi mnamo Januari 21, mwaka huu, kikiwataka watu wanaotaka kuwania urais kupitia chama hicho kuwasilisha maombi yao.

Waliotuma maombi walitakiwa kutimiza matakwa yote yaliyoorodheshwa katika Katiba ya Kenya na katiba ya ODM.

Siku ya mwisho ya kupokea maombi ilikuwa Februari 26 lakini muda huo ukaongezwa hadi Machi 23.

Japo Bw Odinga hajatangaza wazi kwamba atawania urais 2022 lakini dalili zinaonyesha kuwa atakuwa debeni.

Wandani wake, akiwemo nduguye Oburu Odinga, wamedokeza kuwa Bw Odinga atawania urais kwa mara ya mwisho 2022.

Baada ya Bw Odinga kutofautiana na viongozi wenzake wa muungano wa NASA; Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi (ANC), sasa anategemea uungwaji mkono wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, kuna tetesi kwamba huenda Rais Kenyatta akaunga mkono mmoja wa viongozi wa muungano wa Kenya One Alliance (OKA), unaojumuisha Bw Mudavadi, Bw Musyoka, Seneta Wetang’ula na kiongozi wa Kanu Gideon Moi.

Iwapo atapigwa chenga na Rais Kenyatta, wadadisi wanasema, huenda Bw Odinga akalazimika kuungana na Naibu Rais William Ruto.

You can share this post!

Waliokaa jela miaka 22 hatimaye huru

Ghost Mulee asema anapata afueni baada ya ‘shughuli...