• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 10:55 AM
Korti yakubali kesi ya Jowie, Maribe kusikilizwa hadharani

Korti yakubali kesi ya Jowie, Maribe kusikilizwa hadharani

Na HILARY KIMUYU

KESI ya Joseph Irungu, maarufu Jowie, na mwanahabari Jacque Maribe wanaodaiwa kuua mfanyabiashara Monica Kimani itasikilizwa hadharani Mei.

Washtakiwa hao ambao walikuwa wapenzi, Jumatano, waliomba korti isikilize kesi yao hadharani.

Baada ya kutafakari ombi hilo, Jaji Grace Nzioka aliagiza kesi hiyo isikilizwe kuanzia Mei 5, mwaka huu, hadharani kortini.

Bi Maribe na Bw Jowie wamekanusha mashtaka hayo ya kuua Monica usiku wa Septemba 19 na Septemba 20, 2018 ambaye mwili wake ulipatikana bafuni huku ukiwa na majeraha shingoni.

Bi Maribe amekanusha kuhusika na mauaji hayo huku akisema kuwa uhusiano wake na Jowie ulikuwa wa kimapenzi na hawakuwa na njama fiche.

Mnamo 2019, Bi Maribe aliambia korti kwamba masaibu yanayomwandama yanatokana na uhusiano wake wa kimapenzi na Jowie na wala si mauaji ya Monica. “Nilikuwa mpenzi wa Jowie ambaye upande wa mashtaka unadai alihusika na mauaji,” akasema Bi Maribe.

Mashahidi wanne, akiwemo mfanyakazi wa bustani na rafiki wa Bi Maribe tayari wametoa ushahidi wao mbele ya Jaji James Wakiaga, ambaye alihamishwa na jaji mpya akaletwa.

Upande wa mashtaka ulisema kuwa unalenga kuita jumla ya mashahidi 32. Mashahidi wanne wako chini ya ulinzi wa serikali huku watano wakiwa wataalamu, kulingana na mwendesha mashtaka.

Wawili hao walikanusha shtaka la kumuua Monica, 29, na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja.

You can share this post!

Ghost Mulee asema anapata afueni baada ya ‘shughuli...

Nitampigia Rais simu baada ya kujuzwa hali yake na mkewe...