• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
MUTUA: Kinoti arekebishe kosa si kushtumu wanahabari

MUTUA: Kinoti arekebishe kosa si kushtumu wanahabari

Na DOUGLAS MUTUA

MKURUGENZI wa idara ya upelelezi wa jinai (DCI) anapaswa kutuliza boli, akiri kwamba wanahabari wamemnasa akisinzia kazini, afikiche macho na kujirekebisha kimya-kimya.

Bw George Kinoti ameijia juu runinga ya Citizen kwa kutangaza habari fichuzi ambapo baadhi ya polisi wanawauzia na kuwakodisha wahalifu bunduki.

Huku akikanusha maafisa wake wamehusika na uhalifu huo, Bw Kinoti amewaagiza kinyume na sheria wasimamizi wa kituo hicho wafike mbele ya wapelelezi.

Amenikumbusha wakati fulani ambapo idara ya ujasusi – kwa kupagawishwa na fichuzi zilizofanywa na wanahabari – ilitangaza nafasi za kazi na ikasisitiza wanahabari waziombe.

Kwa kutoelewa wanahabari wanavyofanya kazi, idara hiyo iliwaajiri hata walioandika habari za elimu, michezo, hadithi za watoto na burudani kwa jumla!

Sijui mradi huo umefikia wapi kwa kuwa ni miaka zaidi ya 10 tangu uanzishwe, ila nadhani waliobahatika wangali wanakula mishahara ya umma.

Bw Kinoti anapaswa kujua kwamba Wakenya hawajasahau polisi huhusika na visa vya uhalifu, sikwambii kuwapa wahalifu vibali vya kujifanya polisi na kuwakinga wakinaswa.

Hebu kumbuka kisa ambapo Bw Joshua Karianjahi Waiganjo alikamatwa kwa kujidai afisa wa polisi wa cheo cha naibu kamishna kwa miaka mitano mnamo 2013.

Hadi alipotiwa nguvuni, Bw Waiganjo alikuwa ametumikia kikosi cha polisi, akishirikiana na maafisa wa ngazi za juu, kwa jumla ya miaka 10.

Alikamatwa akiabiri helikopta ya polisi, huku kavaa sare rasmi za kikosi hicho, akiandamana na maafisa wakuu kwenda kukagua hali ya usalama kwenye Bonde la Suguta kulikouawa askari kadhaa siku chache zilizotangulia.

Baada ya kubururwa huku na huko na kugongeshwa mwambani kama pweza, Bw Waiganjo aliachiliwa huru na mahakama mwezi Mei mwaka jana ushahidi ulipokosekana.

Kisa kingine ni cha aliyekuwa mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai, siku hizo ikiitwa CID, Bw Joseph Kamau, aliyetuhumiwa kuwapa wahalifu vyeo vikubwa vya polisi.

Wanaokumbukwa zaidi ni mamluki kutoka Armenia, Artur Sargasyan na Artur Margaryan, waliozua vituko kwa vitendo na madai ya kila aina yaliyotishia usalama wa taifa.

Baadaye iliibuka kwamba wawili hao walipiga kambi nchini kwa nia ya kulitwaa shehena kubwa la dawa za kulevya za thamani ya Sh6.4 bilioni lililonaswa na polisi.

Uthubutu ulioje kwa wahalifu hao kufuata mihadarati iliyofungiwa kwenye makao makuu ya polisi wa GSU, Ruaraka, na Chuo cha Mafunzo ya Polisi wa Utawala, Embakasi?

Kwamba walisaidiwa na polisi kupata vibali vya kuwa nchini, vitambulisho vya kuwa manaibu kamishna wa polisi na hata bunduki hatari ili kutenda uhalifu wa kimataifa ni jambo la kutia hofu.

Usisahau Bw Kamau ndiye aliyewaelekeza polisi waliovamia vyumba vya habari vya Nation na Standard vilivyodaiwa kufichua mambo yasiyoifurahisha Ikulu mnamo 2006.

Ni baada ya malalamiko ya Wakenya wa kila tabaka ambapo alisimamishwa kazi kisha tume ikaundwa kumchunguza.

Hatimaye tume hiyo ilimwondolea lawama zote. Bw Kinoti anapaswa kujikakamua kazini na kuelewa wanahabari hawawezi kumjulisha kabla ya kuchunguza lolote. Na hawawezi kumwomba msamaha akisinzia kazini.

[email protected]

You can share this post!

Korti yatupa baadhi ya ushahidi wa mume anayetaka kutaliki...

KAMAU: Viongozi watahadhari wanapopanga kukwamilia mamlakani