• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 AM
KAMAU: Viongozi watahadhari wanapopanga kukwamilia mamlakani

KAMAU: Viongozi watahadhari wanapopanga kukwamilia mamlakani

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Januari 16, 2001, dunia nzima iliamkia habari kuhusu kifo cha ghafla cha aliyekuwa rais wa DRC, Laurent Kabila.

Baada saa chache, ilibainika Kabila aliuawa na mmoja wa walinzi wake kutokana na misukosuko ya kisiasa ambayo ilikuwa ikiendelea nchini humo.

Wakati wa kifo chake, hali nchini humo ilikuwa katika hali ya kuogofya—makumi ya makundi ya wanamgambo yalikuwa yakiwaua mamia ya raia kwenye juhudi za kuteka baadhi ya maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini.

Ingawa msukumo wa kifo chake umebaki kuwa fumbo hadi sasa, baadhi ya nadharia zimekuwa zikieleza walinzi wake walichoshwa na jinsi alivyokuwa akipuuza mahangaiko ya raia, ndipo wakaamua kumuua.

Tukio hilo halikuwa la kwanza kwa rais aliye mamlakani kuuawa ama kulazimishwa kung’atuka uongozini kwa kuonekana kutojali maslahi ya raia wake.

Hata hivyo, lilionekana kujenga imani miongoni mwa raia barani Afrika, kuwa kwa kuungana, wana uwezo kufanya mageuzi ya kiutawala na kisiasa katika nchi zao.

Miongoni mwa nchi zilizoathiriwa ni Kenya, kwani ni baada ya mwaka mmoja tu ambapo Wakenya walipiga kura kwa fujo kukiondoa mamlakani chama cha Kanu, ambacho kilikuwa kimeitawala nchi kwa karibu miaka 40. Wananchi vile vile walikuwa wamechoshwa na utawala wa marehemu Daniel Moi, ambaye kama Kabila, alikuwa akilaumiwa kwa kuyapendelea baadhi ya maeneo nchini kimaendeleo na kuyabagua yale mengine.

Wimbi hilo lilifuatiwa na mageuzi mengine ya kisiasa yaliyoshuhudiwa katika nchi kama Tunisia, Misri, Libya, Burkina Faso na Sudan. Mageuzi ya juzi zaidi yalitokea Jumapili nchini Chad, wakati aliyekuwa rais wa taifa hilo, Idriss Deby, aliuawa katika hali tatanishi kwenye operesheni ya kijeshi kuwakabili wanamgambo.

Kabla ya mauaji hayo, Deby alikuwa ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa urais kwa awamu ya sita, hilo likimaanisha angeendelea kulitawala taifa hilo baada ya kuchukua uongozi mnamo 1990.

Deby alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa wametawala kwa muda mrefu barani Afrika, huku utawala wake ukilaumiwa kwa kuwahangaisha viongozi wa upinzani, vyombo vya habari na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Kama Kabila, mauaji yake pia yamebaki kuwa fumbo. Hata hivyo, kuna madai aliuawa na wanajeshi waliochoshwa na utawala wake.

Bila shaka, mauaji hayo ni funzo kuu kwa marais barani na kwingineko duniani: inafikia wakati raia wanafika mwisho na kufanya maamuzi wao wenyewe.

Tahadharini mnapobuni mikakati ya kuendelea kukwamilia mamlakani.

[email protected]

You can share this post!

MUTUA: Kinoti arekebishe kosa si kushtumu wanahabari

TAHARIRI: Stars ianze kusaka vipaji mashinani