• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
JAMVI: Katika hizi ziara zake Oparanya ni ‘fuko’ au ni mjumbe wa Raila?

JAMVI: Katika hizi ziara zake Oparanya ni ‘fuko’ au ni mjumbe wa Raila?

Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Kakamega Wycliffe Oparanya ameacha Wakenya na maswali tele kutokana na misururu ya mikutano anayofanya na vigogo wa kisiasa nchini.

Baada ya kukutana na Dkt Ruto katika Kaunti ya Narok, Bw Oparanya ambaye ametangaza azma ya kugombea urais kupitia kwa chama cha ODM alikutana na Bw Odinga kumfahamisha aliyojadili na Naibu Rais.

Siku chache baada ya kukutana na Naibu Rais William Ruto, naibu kinara huyu wa chama cha ODM alikutana na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye ametangaza kuwa chama chake kitaondoka katika muungano wa NASA ambao chama cha chungwa ni mwanachama.

Wiper ni mwanachama wa muungano mpya wa One Kenya Alliance unaoshirikisha vyama tanzu vya NASA- Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Moses Wetangula na Kanu cha seneta wa Baringo Gideon Moi.

Katika mkutano wake na Bw Odinga, Bw Oparanya aliandamana na waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa.

Hatua hii imeibua maswali kuhusu iwapo gavana huyo anayehudumu kwa kipindi cha pili anawakilisha maslahi yake binafsi, yale ya chama cha ODM au ya Dkt Ruto.

Baadhi ya duru za kisiasa zinadai kwamba uwepo wa waziri Wamalwa katika mkutano wa gavana huyo kunaashiria mpango mpana wa kisiasa.

Mnamo Jumanne, Bw Oparanya alisema kwamba akiwa mwaniaji wa urais kwenye uchaguzi mkuu, ana uhuru kwa kuzungumza na vigogo wengine wa kisiasa nchini kwa lengo la kuunda muungano wa kisiasa.

“Ninanuia kugombea urais na kwa hivyo nitakuwa nikikutana na viongozi wengine wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022,” alisema siku moja kabla ya kukutana na Bw Musyoka.

Haya yalijiri baada ya kubainika kuwa alikuwa amekutana na Dkt Ruto mara kadhaa kabla ya mkutano wao wa Narok.

Akihojiwa na runinga ya Citizen wiki jana, Dkt Ruto alikiri kwamba amekutana na gavana huyo mara tano na kwamba amevutiwa na kampeni yake ya kusaidia maskini kujiinua kiuchumi.

Dkt Ruto alikanusha madai kwamba Bw Oparanya alikuwa ametumwa kwake na Bw Odinga kumrai waungane kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Duru kutoka kambi ya Dkt Ruto zinadai kwamba Bw Oparanya anapanga kuhama ODM ili kujiunga na Ruto, madai ambayo Oparanya amekanusha kwa kinywa kipana.

Hata hivyo, Bw Oparanya anasema hakuna kinachomzuia kuzungumza na Dkt Ruto au kiongozi yeyote wa kisiasa nchini.

“Ruto ni rafiki yangu na Wakenya wanafaa kuruhusu viongozi kujieleza na kuwa huru kuzungumza,” alisema.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba akiwa naibu kiongozi wa ODM, kuna uwezekano mkubwa kwamba Bw Oparanya anawakilisha kiongozi wake Bw Odinga katika juhudi za kujenga muungano mkubwa wa kisiasa kabla ya 2022.

You can share this post!

JAMVI: Utata wa BBI tishio kwa Handisheki

Betis wadidimiza matumaini ya Real Madrid kuhifadhi ufalme...