• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
JAMVI: IEBC yawaniwa kutekwa nyara kabla ya kura 2022

JAMVI: IEBC yawaniwa kutekwa nyara kabla ya kura 2022

Na CHARLES WASONGA

HAMU ya vigogo wa kisiasa ya kutaka kudhibiti Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia ndicho kiini cha mivutano inayoshuhudiwa katika mchakato wa kuteua wanachama wa jopo litakaloteua makamishna wapya wa tume hiyo.

Hali hii, kwa mujibu wa wadadisi, ni kwa sababu makamishna wanne wapya watashirikiana na watatu walioko sasa (Wafula Chebukati, Profesa Abdi Guliye na Boya Molu) kusimamia uchaguzi huo ambao unatarajiwa kushuhudia ushindani mkubwa. Aidha, watasimamia kura ya maamuzi kuhusu mswada wa BBI inayotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Kwa mujibu wa Sheria ya IEBC iliyofanyiwa marekebisho 2020, Chama cha Wanasheria Nchini (LSK), Baraza la Madhehebu Nchini (IRCK) na Tume ya Huduma za Bunge (PSC) zinahitajika kuteua wawakilishi katika jopo hilo siku saba baada ya nafasi nne za makamishna wa IEBC kutangazwa kuwa wazi.

LSK inahitajika kuteua mwakilishi mmoja, IRCK itateu wawakilishi wawili huku PSC ikiteua watu wanne; wanaume wawili na wanawake wawili, kulingana na sheria hiyo.

Mnamo Aprili 14, 2021 Rais Uhuru Kenyatta alitangaza rasmi nafasi nne katika tume hiyo kuwa wazi na ambazo zitahitaji kujazwa. Nafasi hizo zilikuwa zikishiliwa na Dkt Paul Kurgat, Margaret Mwachanya, Consolata Nkatha na Roselyn Akombe ambao walijiuzuli baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Hii ina maana kuwa LSK, IRCK na PSC zinahitajika kuwa zimeteua wawakilishi wao katika jopo hilo ambapo majina yao yatawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa uteuzi siku 21 baada ya nafasi za makamishna kutangazwa kuwa wazi. Hii ina maana kwamba majina ya wanachama saba wa jopo hilo yatahitajika kuwa yamechapishwa katika gazeti rasmi la serikali kabla au mnamo Mei 5, mwaka huu.

Lakini kufikia Jumamosi, mzozo ulikuwa ungali unatokota katika LSK kuhusu suala hili baada ya mirengo miwili katika chama hicho kuwasilisha majina tofauti. Mrengo wa Rais wa chama hicho Nelson Havi ulimteua Morris Mutua Kimuli huku ule wa Afisa Mkuu Mtendaji Nancy Wambua, unaodai kupata idhini kutoka kwa wanachama wanane wa LSK, ukimteua Bi Dorothy Jemator.

Bw Havi alisema kuwa Bi Jemator hatafanya uamuzi huru kwa sababu “ana uhusiano wa karibu na vyama vya Jubilee na ODM”.

Lakini Bi Wambua amepuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa Bi Jemator ndiye aliibuka bora miongoni mwa mawakili 39 waliotuma maombi ya kutaka nafasi hiyo.

“LSK ilitangaza nafasi hii mnamo Aprili 16 na wanachama 39 wa LSK wakatuma maombi. Mchujo ulipofanywa mbele ya wanachama wanane wa Baraza la LSK, Bi Jemator ndiye alishinda na ndiye tutawasilisha jina lake kwa PSC. Chaguo la Havi na washirika wake hakuchaguliwa kwa kuzingatia utaratibu wa sheria za LSK,” Bi Wambua akaongeza.

Mgawanyiko pia umeibuka katika Baraza la Madhehebu Nchini (IRCK) baada ya kuteuliwa kwa mwenyekiti wake, Kasisi Joseph Mutie na Abdullah Fariduun ambaye ni Muislamu wa imani ya Shia. Kasisi Mutie ni Katibu Mkuu wa Shirika la Makanisa Afrika (OAIC).

Duru zilisema kuwa viongozi wa madhehebu makubwa nchini wamelalamikia uteuzi wa wawili hao kuwa wanachama wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC, wakisema “hawatawakilisha maono ya walio wengi.”

Kwa upande wake, tume ya PSC ilisema kuwa tayari imeteua wawakilishi wake wanne na kuwasilisha majina yao kwa asasi husika.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ambaye ni mwenyekiti wa tume hiyo hata hivyo, hakufichua majina ya watu hao wanne ila akatoa hakikisho kwamba “wanawakilisha masilahi ya mirengo yote ya kisiasa katika Bunge la Kitaifa na Seneti.”

Lakini Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alionya PSC kwamba sharti ihakikishe kuwa nafasi hizo nne zinaendea mirengo yote mikuu ya kisiasa nchini.

“Sisi kama One Kenya Alliance tunataka kupewa nafasi sawa na wenzetu wa Tangatanga, Kieleweke na wengine kutoka vyama vidogovidogo. Hilo lisipofanyika tutaungana kupinga orodha hiyo ya PSC,” akatisha.

Hata hivyo, kulingana na Bw Martin Andati mivutano ambayo imeanza kuibuka katika mchakato wa uteuzi wa wanachama wa jopo la kuteua makamishna wapya ni ishara tosha kwamba vigogo wa kisiasa wanapania kudhibiti tume IEBC kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

You can share this post!

JAMVI: Kibarua kwa Ruto Mlimani Tangatanga wakitunga...

Chelsea wapiga West Ham United na kuingia ndani ya nne-bora...