• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Msichana akiri kubadilisha vipimo vya mimba kuokoa aliyemnajisi

Msichana akiri kubadilisha vipimo vya mimba kuokoa aliyemnajisi

Na STEPHEN ODUOR

Familia moja enee la Tana Delta imeachwa na mshtuko baada ya kugundua kwamba mtoto wao ambaye alikuwa amenajisiwa aliharamisha vipimo vya ujauzito ili kumlinda mhalifu ambaye ni mchumba wake asikamatwe.

Kulingana na nyanya wa msichana huyo ambaye amekuwa akishinikiza haki itendeke, mwanafunzi huyo wa darasa la sita, baada ya kugundua alikuwa mjamzito, aliwakabidhi wauguzi katika zahanati ya Garsen, sampuli ya mkojo ya rafiki yake.

Ajuza huyo alisema ilimjia tu kwamba msichana huyo ambaye pia ni yatima alikuwa na ujauzito baada ya afisa kutoka shirika la Moving The Goal Post na Chifu wa Salama kuamua kufuata uvumi uliokuwa ukienea katika kijiji hicho.

“Tulikuwa tumeripoti kesi hii katika kituo cha polisi cha Gamba na ilikuwa ikichunguzwa wakati mhalifu alipotoweka ghafla. Uchunguzi wa ujauzito kutoka hospitalini ulionyesha hakuwa na mimba na ni sawia na kile tulichoandikisha katika ripoti ya polisi,” alisema .

Wakati huo huo, uvumi uliendelea kuenea katika kijiji hicho na kumfanya msichana huyo kudhoofika kiafya. Hapo ndipo Bi Esther Baya, afisa wa MTG alipomlazimisha msichana huyo kupimwa tena ujauzito chini ya usimamizi wake binafsi katika zahanati ya eneo hilo, vipimo vilivyothibitisha alikuwa na ujauzito wa miezi miwili.

Kabla ya matokeo, msichana huyo alimwita kando afisa huyo wa MTG na kukiri kuwa tayari aliyajua matokeo kwani hapo awali alikuwa amepimwa mara tatu akiwa pamoja na mhalifu.

“Aliniambia tunapoteza muda mwingi kufanya vipimo, tayari alikuwa na matokeo hata kabla ya kupimwa mara ya kwanza na hakutaka kusababisha hofu nyumbani akisema ni chaguo lake kupata ujauzito,” alisema Bi Baya.

Msichana huyo alikiri kupata sampuli ya mkojo kutoka kwa rafiki yake kabla ya kuondoka nyumbani, ambao aliwasilishwa kwa kituo hicho kwa vipimo.

Msichana huyo pia alikiri kumwarifu mshukiwa kuhusu mipango ya kukamatwa kwake. na kumshauri atoroke.

“Kwa hivyo wakati tulikuwa tunahangaika kumtafutia haki, walikuwa hatua moja mbele yetu. Wakati tulikuwa tunarekodi taarifa polisi, walikuwa tayari wamepanga kutoroka,” alisema Chifu Peter Jillo.

Msichana huyo pia anadaiwa kumtishia nyanyake kuwa naye pia angetoweka iwapo mhalifu atakamatwa na kusababisha bibi huyo kutaka mazungumzo na familia ya mhalifu ili kutatua suala hilo katika ngazi ya familia.

Chifu wa eneo hilo baada ya kufahamishwa kuhusu mkutano huo alivamia ukumbi huo na kutawanya mkutano huo, na kuwaonya wazazi husika kutohujumu taratibu za kisheria.

Chifu Jilo alielezea Taifa Leo kwamba visa vya waathiriwa wa unajisi wanaowalinda wahalifu vinaongezeka katika vijiji vya Wema, Hewani na Kulesa huko Tana Delta, huku wazazi wakizitumia kesi hizo kama vitega uchumi.

You can share this post!

SIASA NI UTUMWA TU – KIRAITU MURUNGI

Kilio serikali za kaunti zikikosa kulipa mishahara