• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Nyoro, Wamatangi walaumiana kuhu utafunaji wa pesa za corona

Nyoro, Wamatangi walaumiana kuhu utafunaji wa pesa za corona

Na KAMAU MAICHUHIE

MZOZO wa uongozi umechipuka kati ya Gavana wa Kiambu, James Nyoro, na Senata Kimani Wamatangi kuhusu madai ya ufujaji wa zaidi ya Sh300 milioni za kupambana na janga la Covid-19 katika kaunti hiyo.

Katika kipindi cha wiki moja, wawili hao wamerushiana cheche za maneno huku Bw Wamatangi akimtaka Gavana Nyoro aeleze jinsi serikali yake imetumia fedha hizo.

Kwa upande wake, gavana huyo amemsuta seneta huyo akidai anatumia wajibu wake kuendeleza siasa za mwaka wa 2022.

Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilifichua hitilafu katika matumizi ya Sh328 milioni.

Ilibainika kuwa sehemu kubwa ya pesa hizo zilitumika bila mipango ya kazi, kutoa malipo maradufu na ununuzi wa vifaa vya kimatibabu vya thamani ya Sh8.9 milioni kinyume cha sheria.

Bw Wamatangi, ambaye pia ndiye Kiranja wa Wengi katika Seneti, anashikilia kuwa sharti Gavana Nyoro awajibikie pesa hizo.

“Tunataka Gavana Nyoro aeleze ni nani alifuja pesa za kaunti. Japo pesa kidogo zilitumika vizuri na kazi inaonekana, wapi hizo zingine ambazo haziwezi kuwajibikiwa? Mbona watu wengine wanalipwa mishahara na marupurupu mara sita?” Seneta aliuliza jana.

Aliongeza: “Hatutamsamehe mtu yeyote aliyeiba pesa za umma wakati huu wa janga la Covid-19. Kuna wale wanaodhani wanaweza kufyonza pesa za umma kwa sababu shughuli zilikuwa zikiendeshwa kwa dharura; tutawaandama hadi mwisho!”

Lakini Gavana Nyoro, ambaye amekosolewa na baadhi ya viongozi wa kaunti kutokana mtindo wake wa uongozi, anasema Bw Wamatangi anaongozwa na siasa pamoja na chuki katika ukosoaji wake.

“Ingawa hajatangaza nia ya kuwania ugavana, dalili zaonyesha kuwa atajitosa kwenye kinyang’anyiro, na anatumia nafasi yake katika Seneti kuniwekea lawama,” akasema Bw Nyoro.

Gavana Nyoro alisema Bw Wamatangi hakupaswa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Seneti kuhusu Afya wiki jana, ambapo alidadisiwa kuhusu matumizi ya fedha hizo za kupambana na Covid-19.

“Wamatangi angejiondoa kutoka kamati hiyo kwa sababu anatoka Kiambu, na pia atakuwa mshindani wangu katika uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema.

Gavana Nyoro na Seneta Wamatangi walirushiana cheche za maneno wakati wa mkutano huo ulioendeshwa kwa njia pepe ya mtandao.

Bw Wamatangi alimtaka gavana kueleza wanachama wa kamati, inayooongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito, kwanini serikali yake ilitumia karibu asilimia 80 ya mgao wake kulipa mishahara ya wafanyakazi.

“Mbona serikali ya Kiambu, ambayo hupokea Sh12 bilioni kwa wastani kila mwaka kutoka kwa Hazina ya Kitaifa, hutumia Sh2 bilioni pekee katika maendeleo?” akataka kujua Seneta huyo.

Lakini Gavana Nyoro alimjibu Ijumaa katika uwanja wa michezo wa Kiringiti akisema: “Haifai kuketi hapo kama seneta ili uulize maswali yanayoikosoa serikali yangu ilhali tunafahamu kwamba unataka kuwania kiti cha ugavana.

“Tunakualika hapa uwanjani sababu hapa ndipo siasa huchapwa. Tukomeshe siasa katika Seneti; tulete siasa hapa Kiambu. Sitakubali kuangushwa kwa njia hiyo,” akasisitiza Bw Nyoro.

You can share this post!

Knut yasaka pesa za kuandaa kongamano la wajumbe

King’ang’i na wanahabari tisa waachiliwa baada...