Wezi wa mifugo sasa wageukia teknolojia kuiba, kuhepa polisi

BARNABAS BII Na FLORA KOECH

Majangili katika maeneo yanayoathiriwa na visa vya wizi wa mifugo Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wamegeukia teknolojia kutekeleza mashambulizi na kukwepa walinda usalama.

Wavamizi hao kutoka jamii za wafugaji Kaskazini mwa Kenya, kwa muda mrefu, wamekuwa wakichukuliwa kama wasio na kisomo wala ujuzi wa kiteknolojia.

Hata hivyo, wamebadilisha mbinu na kuanza kutumia huduma za simu na mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, kuitisha msaada wakati wa mashambulizi, na kuwasiliana na jamaa zao wanaoishi maeneo ya mijini wanaowasambazia vifaa. “Simu zimegeuka kuwa vifaa mwafaka huku wavamizi wakibuni mbinu mpya za kutekeleza mashambulizi. Hii inafanya kuwa vigumu kwa maafisa wa usalama kuwanasa majambazi,”alisema Bw Mark Ajon Lokwawi, kutoka Lokiriama, Loima, Kaunti ya Turkana.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika kaunti za Turkana na Pokot Magharibi, ulifichua kuwa wachungaji wengi, hususan vijana kati ya umri wa miaka 18-40 wanamiliki simu.

“Vijana wengi wanatumia teknolojia. Wanatumia mitandao ya kijamii kama vile makundi ya WhatsApp kuendeleza maslahi yao ikiwemo kupanga uvamizi na kukwepa kikosi cha usalama,” alisema Bw Esekon Ekiru, mtetezi wa haki za kibinadamu Mjini Lodwar.

“Wavamizi hao wanatumia ujanja kwa kutumia simu kupanga mashambulizi na uvamizi. Huwasaidia kuwasiliana na viongozi wao na kutambua mahali ambapo mifugo wanalishwa,” alisema Bw Ekiru.

Alihusisha mashambulizi mabaya yaliyosababisha mapigano ya jamii za wafugaji na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na wasomi kutoka jamii zinazopigana.

“Baadhi ya watu, hasa kutoka maeneo ya mijini, hutumia mitandao ya kijamii kuchochea jamii jambo linalosababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi,” alisema Bw Ekiru. Wapiganaji hutumia simu kupokea jumbe kuhusu masuala yanayoendelea ikiwemo mipango ya serikali ya kutekelea oparesheni za kuwapokonya wahalifu silaha.

“Matumizi ya digitali yamewezesha watu kupata habari kutoka maeneo kama hayo ya mashinani kabisa ambapo ni vigumu kupata gazeti,” alisema Zablon Natieng, kutoka Natira, Turkana Magharibi.

Katika eneo linalokabiliwa na ukosefu wa usalama la Kapedo, kwenye mpaka wa Turkana Mashariki na Tiaty, hali ya utulivu imeanza kurejea baada ya Safaricom kuweka vituo na minara ya mawasiliano, ili kuimarisha mtandao wa mawasiliano na kurahisisha kazi maaafisa wa usalama.

Mnara wa Safaricom kwenye vilima vya Silale na eneo la Tiaty na Napeitom, Turkana Mashariki umerahisisha upigaji simu kuitisha msaada kutoka kwa maafisa wa usalama wakati wa mashambulizi.