• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Corona: Idadi ya waliopokea chanjo duniani yafika bilioni

Corona: Idadi ya waliopokea chanjo duniani yafika bilioni

Na AFP

IDADI ya watu waliopokezwa chanjo ya corona kote duniani imefikia bilioni moja. Takwimu zinaonyesha kuwa chanjo ya corona imetolewa katika nchi 207.

Hata hivyo, asilimia 58 ya chanjo imetolewa katika nchi tatu pekee; Amerika (watu milioni 225), China (milioni 216) na India (milioni 138).

Lakini kwa kuangalia idadi ya watu; Israeli inaongoza kwa kutoa chanjo kwa idadi kubwa ya raia wake. Watu sita kati ya 10 wamedungwa chanjo nchini Israeli.

Milki ya Falme za Uarabuni (UAE) inafuatia kwa kudunga asilimia 51 ya raia wake, Uingereza (asilimia 49), Amerika (asilimia 42), Chile (asilimia 41), Bahrain (asilimia 38) na Uruguay (asilimia 32).

Asilimia 21 ya raia wa mataifa ya Umoja wa Ulaya (EU) wamedungwa chanjo ya corona.

Asilimia 22 ya raia wa Ujerumani wamedungwa chanjo ya corona nchini Ujerumani, Uhuspania (asilimia 20), Ufaransa (asilimia 20) na Italia (asilimia 20).

Kasi ya utoaji wa chanjo kote duniani imeongezeka maradufu ndani ya mwezi mmoja uliopita, kulingana na takwimu za AFP.

Nchi maskini, haswa mataifa ya Afrika, zinazonufaika na chanjo nafuu kupitia mpango wa Covax, zimetumia asilimia 47 ya chanjo zilizopewa.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) mataifa maskini yanayopata chanjo kupitia Covax yamedunga asilimia 0.2 ya raia wake. Kenya ni miongoni mwa mataifa yanayonufaika na chanjo kupitia mpango wa Covax.

Mataifa 12 hayajaanza mchakato wa kutoa chanjo kwa raia wake. Mataifa hayo ni Tanzania, Madagascar, Burkina Faso, Chad, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Eritrea.

Mengine ni Vanuatu, Samoa and Kiribati, Korea Kaskazini na Haiti.

Katibu Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus ameelezea wasiwasi wake kuhusu ukosefu wa usawa katika utoaji wa chanjo katika nchi zote.

“Katika mataifa yaliyostawi kiuchumi karibu mtu mmoja kati ya wanne amedungwa chanjo. Lakini katika mataifa maskini ni mtu mmoja kati ya 500,” akasema Tedros.

Chanjo ya iliyotengenezwa na kampuni ya AstraZeneca kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Oxford, ndiyo imetolewa kwa wingi zaidi katika nchi 156.

Chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya Pfizer kwa ushirikiano na BioNTech inatolewa katika mataifa 91 huku Moderna ikitolewa katika nchi 46.

Chanjo ya Sinopharm inatolewa katika nchi 41 huku chanjo ya Sputnik V ya nchini Urusi ikitolewa katika mataifa 32. Chanjo ya Sinovac iliyotengenezewa nchini China inatolewa katika mataifa 21.

Maambukizi ya virusi vya corona, hata hivyo, yanazidi kuongezeka kote duniani. Watu zaidi ya milioni 3.1 wamethibitishwa kufariki kote duniani kutokana na maradhi ya corona.

You can share this post!

Gavana Nyong’o hatarini kukamatwa kwa kukaidi seneti

Siraj Mohamed sasa atia bidii kuichezea Harambee Stars