• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
VALLARY ACHIENG: Ipo siku mtanitazama kwa runinga

VALLARY ACHIENG: Ipo siku mtanitazama kwa runinga

Na JOHN KIMWERE

MWANZO wa ngoma kila mja hujipa matumaini ambapo huwa ni hali ya kutarajia. Ni katika kutumainia na kuvumilia ambapo ana imani nyota yake itang’aa na kuibuka msanii wa kimataifa miaka ijayo.

Vallary Pascal Achieng maarufu Saumu ni miongoni mwa waigizaji wanaolenga kujituma kisabuni kuhakikisha wanatinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

Binti huyu aliyetua duniani 1997 amehitimu kwa shahada ya diploma kama mwana habari wa Televisheni na Redio kwenye chuo Kikuu cha Daystar University.

Kisura huyu anasema kuwa alianza kujituma katika masuala ya uigizaji mwaka 2018 akifanya na Kumbo Media Production.

”Katika mpango mzima tangia utotoni mwangu nilikuwa napenda kushiriki michezo ya kuigiza. Nilivutiwa na maigizo baada ya kutazama filamu iitwayo ‘Aziza’ aliyoshiriki msanii mahiri Sanaipei Tande,” alisema na kuongeza kwamba anatamani sana kuibuka kati ya wasanii wanaovuna pesa ndefu nchini.

Ingawa bado hajapata mashiko katika tasnia ya maigizo anasema kuwa anaamini anauwezo tosha kufanya vizuri maana amepania kuibuka mwana maigizo shupavu nchini.

Msichana huyu anasema ingawa kazi zake hazijafanikiwa kupata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga yoyote nchini anajivunia kushiriki filamu kadhaa ndani ya miaka miwili iliyopita.

Ameshiriki filamu kama Izraili na Kituko (zote Kumbo Media Production), Traggic Vallentine na Secret Lover (zote M Jey Production).

INI EDO

Dada huyu anachukulia uigizaji kama ajira ambapo anataka kuibuka msanii maarufu nchini ndani ya miaka mitano ijayo.

Mwigizaji huyu angependa sana kufanya kazi na wenzake wanaofanya kweli hapa nchini kama Sarah Hassan aliyeshiriki filamu kama ‘Crime and Justine,’ na ‘Zora.’

Kwa wasanii wa kigeni anataka kujikuta jukwaa moja na Leleti Khumalo wa Afrika Kusini aliyeigiza filamu kama ‘Sarafina,’ na ‘Yesterday.’ Pia yupo msanii wa filamu za Kinigeria (Nollywood), Ini Edo aliyefanya kazi kama ‘Palace Maid,’ na ‘Married to the enemy,’ kati ya zingine.

MAWAIDHA

Chipukizi huyu anashauri wenzake wajitume kiume bila kulegeza kamba wala wasiwe na hofu mradi wajiamini wanaweza. ”Pia ningependa kuwahimiza kuwa wasikubali kushushwa hadhi na wanaume bali wazingatie azma yao,” akasema.

Pia anatoa wito kwa maprodusa wa humu nchini waache mtindo wa kudharau wasanii chipukizi badala yake wawakuze ili kutwaa nafasi za wenzao waliokamaa watakapoondoka duniani.

CHANGAMOTO

Anasema huwa vigumu kwa waigizaji wanaokuja kupata nafasi za ajira maana maprodusa wengine hupenda kuwapa nafasi wenzao waliowatangulia.

”Binafsi ningependa kutoa mwito kwa wenzetu waliokomaa katika sekta ya uigizaji watushike mkono ili tupaishe jukwaa la maigizo nchini na kutoa ajira kwa chipukizi waliofurika katika kila kona ya taifa hili,” akasema.

You can share this post!

Rufina (Mama Silas) aelezea safari yake ya uigizaji

ERICK GUTO: Nimeshiriki filamu nyingi ila Hullabaloo ndiyo...