• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Mvutano kati ya Ottichillo na naibu wake wachacha

Mvutano kati ya Ottichillo na naibu wake wachacha

Na DERICK LUVEGA

MVUTANO kati ya Gavana wa Vihiga Wilber Ottichillo na naibu wake, Dkt Patrick Saisi, unaendelea kuchacha.Hii ni baada ya Dkt Saisi kutangaza kuwa atatoa rasmi mwelekeo wake wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, 2022.

Naibu gavana huyo aliwaambia wafuasi wake kwamba mwezi ujao ataweka wazi kiti atakachowania. Bw Ottichillo na Dkt Saisi wamekuwa wakizozana tangu mwezi Februari kuhusu mgomo wa madaktari, ambao umekuwa ukiendelea tokea Desemba mwaka jana.

Dkt Saisi alifanya makubaliano na madaktari ambapo alisaini mkataba wa kurudi kazini ili wahudumu hao wamalize mgomo.Hata hivyo, Gavana Ottichillo akapuuzilia mbali maafikiano hayo.

Dkt Saisi alihisi kwamba Gavana alimdunisha kisiasa, hasa baada ya kumtaka ajiuzulu.Uhasama baina yao pia ulitoneshwa na matamshi ya Naibu Gavana yapata miezi miwili iliyopita, kwamba yeye na Bw Ottichillo hawawezi kushirikiana kwa sababu uongozi wao unatofautiana.

Ili kuondoa madai yanayoenea kuhusu ushirikiano wake na gavana wa zamani Bw Moses Akaranga, Dkt Saisi alisema kuwa mkuu huyo wa zamani wa kaunti ni rafiki tu.

“Huwa tunakutana na Bw Akaranga kwenye hafla mbalimbali kama vile za mazishi na kutazama mechi za kandanda,” alihoji Bw Saisi.

Vile vile, alidokeza kuwa yeye hushauriana mara kwa mara na kiongozi wa chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi, na Mbunge wa Sabatia Bw Alfred Agoi ambao anasisitiza pia ni marafiki zake.

You can share this post!

Karua aonya kuhusu njama ya kuahirisha kura

Orengo apendekeza Oburu Odinga kumrithi useneta Siaya