• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Orengo apendekeza Oburu Odinga kumrithi useneta Siaya

Orengo apendekeza Oburu Odinga kumrithi useneta Siaya

Na CECIL ODONGO

SENETA wa Siaya James Orengo ametangaza kuwa anampendekeza kakake kiongozi wa ODM Raila Odinga, Dkt Oburu Odinga, kurithi kiti cha Useneta wa Siaya kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Orengo ambaye pia alifichua kuwa analenga kujitosa katika mbio za ugavana 2022, alisema mwakilishi huyo katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ana tajriba pevu ya kisiasa na jemedari halisi wa ODM.

Hivyo, anatosha kuwawakilisha wakazi wa Siaya katika Bunge la Seneti.Wakili huyo alisisitiza kuwa Dkt Oginga amesimama pamoja na Bw Odinga wakati wa maamuzi magumu ya kisiasa ndiposa ndiye bora zaidi kuwahi useneta 2022 kuliko wapinzani wake.

“Hao wote wanaokimbia hapa na pale wakisema wanataka useneta, wanafaa wawaeleze wamekuwa wapi wakati Bw Odinga alikuwa akipambana na mawimbi makali ya kisiasa.

“Huyu Oburu amesimama na Baba kila wakati. Alikuwa Uhuru Park tukimwaapisha Baba na amekuwa mwenye hekima kwa kuchangia na kuunga maamuzi magumu ya kisiasa tuliyoyakumbatia kama chama cha ODM,” akasema Bw Orengo.

Mbunge huyo wa zamani wa Ugenya alisisitiza kuwa ashaelekeza macho yake katika kiti cha ugavana na atahakikisha kuwa, pamoja na Dkt Oginga wanamsaidia Bw Odinga kuingia Ikulu 2022.Wakati huo huo, alisema Wakenya wataelekea kwenye referenda mnamo Julai na kukanusha madai kwamba Mswada wa BBI uliofikishwa bungeni wiki jana ulibadilishwa.

“Sitatea wadhifa wangu wa Useneta kwa sababu naomba niwe gavana wenu. Nitashikana na Oburu kumsaidia Kinara wetu afike Canaan,” alieleza mwanasiasa huyo mzoefu na kushikilia kuwa ni kupitia BBI ambapo Bw Odinga ana nafasi nzuri ya kuingia Ikulu 2022.

Dkt Oburu amekuwa akiendeleza kampeni za kichichini za Useneta kwani marufuku ya mikutano bado inaendelea nchini kutokana na janga la corona.Alihudumu kama Mbunge wa Bondo kwa miaka 19 (1994-2013), kisha akahudumu kama Mbunge Maalum kati ya 2013-2017 kabla kuteuliwa kama Mbunge wa Eala.

Atakuwa akijaribu bahati kwa mara ya pili katika kiti cha Useneta kupitia chama cha ODM, baada ya kumuachia Bw Orengo nafasi hiyo mnamo 2013.Japo mwaka huo alilenga useneta, Dkt Oginga alitupilia mbali azma yake kuepuka kivumbi kwenye kura za mchujo za ODM dhidi ya Bw Orengo., kisha akawania mchujo tata wa ugavana dhidi ya mfanyabiashara William Oduol.

Mchujo huo wa ugavana ulifutwa na ODM baada ya Dkt Oginga na Bw Oduol, wote kudai ushindi, kisha Cornel Rasanga akapokezwa tiketi ya moja kwa moja.

Katika juhudi zake za kutwaa ugavana, Bw Orengo naye anatarajiwa kutifua vumbi dhidi mbunge wa Alego Usonga Opiyo Wandayi, aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Mhandisi Nicholas Gumbo kati ya wawaniaji wengine.

You can share this post!

Mvutano kati ya Ottichillo na naibu wake wachacha

Ulipaji fidia kwa wakazi wa Lamu ni kabla ya Juni