• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Uhuru atupa marafiki

Uhuru atupa marafiki

Na BENSON MATHEKA

WALIOKUWA marafiki wa kisiasa wa Rais Uhuru Kenyatta wamesema uhusiano wao na kiongozi wa taifa ulivunjika alipoamua kubadilisha mtindo wake wa uongozi baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Miongoni mwa marafiki hao ni waliokuwa wafuasi sugu wa Rais Kenyatta tangu 2002 alipogombea urais kwa mara ya kwanza, na wengine hata walikuwa wasaidizi wake wa kibinafsi

Wengi wao walikuwa watetezi wake wakuu aliposhtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) pamoja na Naibu Rais William Ruto.

Marafiki hao wa zamani wa rais sasa wanasema walijipata nje ya serikali walipoanza kumkosoa kuhusu mtindo wake mpya wa uongozi baada ya uchaguzi wa 2017, na wengi wao wamelipia gharama kwa kutengwa katika utawala, kufutwa kazi na baadhi kudai kuhangaishwa.

Naibu Rais William Ruto anasema kuwa urafiki wake na rais ulizorota alipoamua kufanya kazi na waliokuwa wapinzani wa Jubilee: “Mtindo wake ulibadilika na ana haki ya kufanya hivyo kwa kuwa ndiye mkubwa. Kwa sababu ya kubadilisha mtindo, nafasi yangu ilichukuliwa na watu wengine.”

Wakati wa kampeni za 2013 na muhula wa kwanza wa serikali ya Jubilee, wawili hao walikuwa marafiki wakubwa, lakini sasa hawaonani uso kwa uso.

Rafiki mwingine wa karibu ambaye aliishia kufutwa kazi ni aliyekuwa waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri, ambaye anasisitiza kuwa masaibu yake yalitokana na yeye kuwa rafiki wa Dkt Ruto: “Kufikia sasa, rais hajaeleza kwa nini alinifuta. Ni haki yake kuajiri na kufuta wakati wowote,” Bw Kiunjuri alisema.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Kenyatta aliwaomba wakazi wa Kaunti ya Laikipia wamruhusu Bw Kiunjuri asigombee ugavana ili amsaidie kama waziri katika serikali ya kitaifa. Lakini muda mfupi baada ya kumteua waziri, rais alianza kumshambulia hadharani na mnamo Januari mwaka jana akamfuta kazi ya uwaziri.

Tangu aliposhtakiwa ICC, Rais Kenyatta alikuwa na uhusiano wa karibu na mwanablogu Dennis Itumbi, na aliposhinda urais 2013 alimteua mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali katika Ikulu. Hata hivyo, mwaka jana yeye na wakurugenzi wengine wa kitengo cha habari za rais walitimuliwa.

Kwa wakati huu, Bw Itumbi amejiunga na Dkt Ruto na amekuwa akikosoa serikali na chama cha Jubilee ambacho alikuwa akitetea vikali.

Bw Itumbi aliambia Taifa Leo kwamba yeye na rais walitofautiana kimawazo lakini anamtambua kama kiongozi wa nchi: “Kuna tofauti za kimawazo na kisiasa kati yetu.”

Aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini, Kabando wa Kabando asema kuwa Rais Kenyatta amesahau safari yake ndefu ya siasa hadi akawa kiongozi wa nchi: “Amekataa kuzingatia maafikiano na viongozi waliounda serikali ya Jubilee, na hiki ndicho chanzo cha kukosana na marafiki wake na kusambaratika kwa umoja wetu. Ninamheshimu sana rais ndiposa mimi humkosoa hadharani na kwa roho safi. Uamuzi ni wake!”

Rafiki mwingine wa rais ambaye amegeuka kuwa mwiba kwake ni Mbunge wa Gatundu Kusini, ambako ndiko nyumbani kwa Rais Kenyatta, Moses Kuria, ambaye uhusiano wao wa kisiasa ulianza tangu utawala wa Kanu. Lakini kuanzia 2018, Bw Kuria amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Kenyatta eneo la Mlima Kenya.

Licha ya Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua kuwa msaidizi wa Rais Kenyatta kuanzia 2001, sasa mwanasiasa huyo kutoka Nyeri ni mmoja wa wakosoaji wakuu wa kiongozi wa taifa.

Bw Gachagua anasema hana uhasama wa kibinafsi na Rais Kenyatta, mbali kilichofanya wakosane ni kutotimiza ahadi yake ya kumuunga mkono Dkt Ruto kuwania urais: “Sina uhasama wa kibinafsi na rais. Tofauti zetu ni za kisiasa kwa kuwa alimruka Dkt Ruto.”

Rais Kenyatta alitofautiana pia na Seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki licha yake kuwa mmoja wa mawakili wake katika kesi za baada ya uchaguzi mkuu wa 2008 katika ICC.

Prof Kindiki, ambaye ni msomi wa masuala ya kisheria na katiba, ni mmoja wa walioandika katiba ya chama cha Jubilee na kuweka mikakati iliyokifanya kushinda uchaguzi mkuu wa 2017.

Katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Kenyatta, Prof Kindiki alikuwa kiongozi wa wengi katika Seneti kabla ya kuteuliwa naibu spika baada ya uchaguzi mkuu wa 2017. Lakini mwaka jana alitofautiana na rais kwa kumuunga mkono Dkt Ruto, ndiposa akapokonywa wadhifa huo.

Wengine waliokuwa marafiki sugu na watetezi wakuu wa Rais Kenyatta lakini sasa wamekosana naye kisiasa ni waliokuwa magavana Mike Sonko (Nairobi), Ferdinand Waititu (Kiambu), maseneta Irungu Kang’ata wa Murang’a, Susan Kihika (Nakuru) na Kipchumba Murkomen (Elgeyo-Marakwet) pamoja na wabunge kadhaa.

Akionekana kujitetea kwa kuhepwa na marafiki zake, Rais Kenyatta alisema mnamo 2018: “Heri tupoteze marafiki. Tutapata wengine na kusonga mbele.”

You can share this post!

Wakenya wamwomboleza Philip Ochieng’

Naibu Rais alenga kuwarai mabwanyenye wa Mzee Moi wamuunge...