• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Rais Suluhu aachilia huru wafungwa 5,001

Rais Suluhu aachilia huru wafungwa 5,001

NA THE CITIZEN

RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaachilia wafungwa 5,001 waliokuwa wakitumikia vifungo mbalimbali katika magereza tofauti kote nchini humo.

Miongoni mwa wafungwa hao, 1,516 waliachiliwa baada ya robo ya muda wa kifungo walichokuwa wakitumikia gerezani kupunguzwa kuambatana na kipimo rasmi cha kupunguza thuluthi moja katika Kifungu 58 cha Sheria za kuhusu Magereza nchini Tanzania.

Wafungwa 3,485 ambao vifungo vyao vilipunguzwa wataendelea kutumikia muda uliosalia gerezani kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Gerson Msigwa.

Rais Suluhu, kupitia taarifa hiyo, aliwahimiza wafungwa wote walioachiliwa kutumia vyema mafunzo waliyopokea walipokuwa gerezani na kuungana na raia wenzao katika ujenzi wa taifa huku wakiheshimu na kuzingatia sheria za taifa.

‘Ningependa pia kuwahimiza Watanzania kutumia maadhimisho ya 57 ya Siku ya Muungano kutafakari kuhusu juhudi kadhaa zilizofanikishwa katika ujenzi wa taifa pamoja na wajibu wa kila mtu katika kuendelea kujenga taifa imara,” alisema Kiongozi huyo wa taifa.

Aidha, rais huyo aliahidi kuendelea kutunza, kulinda na kuendeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa manufaa ya raia wa Tanzania kutoka pande zote.

You can share this post!

Naibu Rais alenga kuwarai mabwanyenye wa Mzee Moi wamuunge...

Safari ndefu ya mwanachuo kusaka maisha bora baada ya...