• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
Gavana aliyeachia mke mamlaka ang’olewa uongozini licha ya amri ya korti

Gavana aliyeachia mke mamlaka ang’olewa uongozini licha ya amri ya korti

Na CHARLES WANYORO

GAVANA wa Wajir, Mohammed Abdi, amebanduliwa katika nafasi hiyo na bunge la kaunti hiyo.Madiwani 37 walipiga kura ya kutokuwa na imani naye huku 10 wakimtetea nao wawili wakakosa kufika bungeni.

Uamuzi wao ulijiri hata baada ya mahakama kuu ya Meru kutoa amri ya kuwazuia madiwani hao dhidi ya kujadili hoja ya kumuondoa uongozini.

Jaji Edward Muriithi alitoa amri hiyo huku akisema kuwa korti itatoa mwelekeo kuhusu suala hilo mnamo Alhamisi kwa pande zote.

Wakazi wa Wajir Aden Ibrahim Mohammed, Omar Jele Abdi, Bishar Ahmed Hussein, Safiya Mahamed Abdi na Yussuf Ibrahim Dimbil ndio walieleza kortini kupinga kujadiliwa kwa hoja ya kumtimua gavana wao.

Jaji Muriithi aliwaagiza wanne hao kufikisha hati ya amri yake kwa karani wa Bunge la Wajir Shalle Sheikh, Spika Ibrahim Ahmed na diwani wa Tulatula Abdullahi Isaack ambaye ni mwasilishaji wa hoja hiyo.

Notisi ya kutimuliwa kwa Bw Mohammed ilitolewa Aprili 19 na kupitia mawakili Ndegwa Njiru na Mugambi Kiogora, anataka Bw Isaack asiwasilishe hoja hiyo wala isijadiliwe hadi kesi isikizwe na iamuliwe.

Bw Njiru alisema Gavana huyo atakuwa ameonewa iwapo mahakama itaruhusu atimuliwe ilhali mchakato wa kisheria haukufuatwa.

Wakili Njiru pia alimshutumu Spika Ahmed kwa kupendelea upande unaomtaka Gavana atimuliwe ilhali kikatiba hafai kuegemea upande wowote.

“Notisi inaweza kutolewa na diwani aliyeteuliwa na Spika wala si Spika mwenyewe,” akasema Bw Njiru.Wakili huyo alisisitiza Bunge la Kaunti halikudhihirisha kuwa hoja hiyo inaungwa mkono na theluthi ya madiwani wala hakukuwa na ushirikishaji wa umma.

You can share this post!

Safari ndefu ya mwanachuo kusaka maisha bora baada ya...

Shughuli za ardhi kufanyika kidijitali