• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Shughuli za ardhi kufanyika kidijitali

Shughuli za ardhi kufanyika kidijitali

NA PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta jana alizindua mfumo wa dijitali wa kusimamia rekodi za ardhi zikiwemo hati miliki. Mfumo huo unaofahamika kama “ArdhiSasa” utakuwa na rekodi zote za ardhi nchini, ambapo wananchi wataweza kutafuta habari za umiliki wa ardhi, kutuma maombi ya hati miliki, kuuza ardhi na shughuli zingine za mashamba.

Huduma hizo zitapatikana kutumia tovuti ya https://ardhisasa.lands.go.ke/home. “Kwa kuwepo kwa jukwaa la “ArdhiSasa” kuna maana mwisho wa kupotea kwa faili, ulaghai wa kila mara, ufisadi pamoja na shughuli haramu za ardhi.

“Kuzinduliwa kwa mpango huu kutashirikisha na kutoa suluhisho kwa mizozo ya kihistoria ya ardhi pamoja na kutoa hakikisho la usalama na thamani ya hati yako ya umiliki wa ardhi na hivyo kuzingatia wito wa ‘Shamba Lako, Hati Safi,’” akasema Rais Kenyatta.

Kufuatia uzinduzi wa “Ardhisasa”, mfumo wa zamani wa usimamizi wa ardhi jijini Nairobi umeondolewa. Hata hivyo, wamiliki wa ardhi ambao huenda wakose kupata hati zao wanashauriwa kuwa wavumilivu huku Wizara ya Ardhi inapoendelea kuimarisha jukwaa hilo la kidijitali.

“Kaunti nyingine 20 zitajumuishwa kwenye mfumo wa kidijitali kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Tunatarajia kwamba kaunti zote zitanufaika kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2022,” kasema Rais Kenyatta.

Waziri wa Ardhi Faridah Karoney alisema jukwaa hilo la kidijitali litatumika kama kituo cha kutoa huduma na taarifa zote za Serikali kuhusu masuala ya ardhi.

Katibu wa Wizara ya Ardhi, Nicholas Muraguri alisema jukwaa la Ardhisasa litawawezesha Wakenya kuanzisha na kufuatilia shughuli za mashamba wakiwa nyumbani au ofisini kwa kutumia simu au tarakilishi.

You can share this post!

Gavana aliyeachia mke mamlaka ang’olewa uongozini licha...

ODM yawaagiza wabunge wake waipitishe BBI