• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
ODM yawaagiza wabunge wake waipitishe BBI

ODM yawaagiza wabunge wake waipitishe BBI

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimewataka wabunge na maseneta wake kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) kama ulivyo ikionya kuwaadhibu wale watakaoenda kinyume na msimamo huo.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge jana, mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi alipuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa mgawanyiko katika chama hicho kuhusu suala hilo.

“Wale ambao inadaiwa wanapinga baadhi ya mapendekezo kwenye mswada huo wanafanya hivyo kama watu binafsi au wanachama wa kamati ya bunge kuhusu haki na masuala ya sheria (JLAC). Sasa msimamo wa ODM ni kwamba wabunge wetu wote wapitishe Mswada wa BBI kesho (leo) jinsi ulivyo,” akasema.

Seneta wa Siaya James Orengo, mwenzake wa Nyamira Okong’o Omogeni na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo Jumatatu walisema baadhi ya vipengele katika mswada huo vinakiuka katiba.

Watatu hao walitaja kipengele kinachogawa maeneo bunge 70 mapya yanayopendekezwa na mswada huo, wakisema hiyo ni kazi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inavyoelezwa kwenye kipengele cha 89 (4) cha Katiba ya sasa.

“Ni kwa msingi huu ambapo nimetia sahihi ripoti ya kamati ya pamoja ya sheria ambayo imebaini dosari hii na zingine zilizoko katika mswada huo. Wataalamu waliandika mswada huu walikosema kwa kugawanya maeneo mapya kwa hii ni kazi ya IEBC,” akasema Bw Amollo, ambaye ni naibu mwenyekiti wa bunge inayosimamia utekelezaji wa katiba (CIOC).Lakini jana, Bw Mbadi alitaja msimamo huo kama ya “watu binafsi” bali sio wa ODM kama chama.

“Msimamo ambao ninautoa wa chama cha ODM na kiongozi wake Raila Odinga. Kwa hivyo, wabunge, maseneta na wafuasi wetu wote hawana budi kuufuata,” akasisitiza Mbunge huyo wa Suba Kusini.

Bw Mbadi alisema japo ni kweli matakwa yote ya ODM hayakujumuishwa kwenye mswada huo, umesheheni mengi ya yale ambayo chama hicho kilipendekeza kilipowasilishwa memoranda yake kwa jopo la BBI mwaka jana.

“Kwa mfano, tunaonga mkono nyongeza ya mgao wa fedha kwa kaunti hadi ngazi ya wadi, kupigwa jeki kwa vita dhidi ya ufisadi, ugavi sawa wa rasimali, mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi kati ya masuala mengi, uwepo wa usawa wa kijinsia, miongoni mwa mengine,” akaeleza.

Bw Mbadi aliongeza kuwa ODM inaunga mkono mswada wa BBI kwa sababu inapendekeza kubuniwa kwa nyadhifa zaidi katika kitengo cha uongozi pendekezo ambalo alisema litakomesha uwezekano wa kutokea kwa ghasia kila baada ya uchaguzi mkuu.

“Wafuasi wa ODM ndio wamekuwa wakiathirika zaidi kwa kuchapwa na polisi kila baada ya uchaguzi mkuu. Baadhi yao wamepoteza maisha katika fujo kama hizo. Tunaunga mkono mswada wa BBI kwa sababu hatutaki matukio kama hayo kutokea tena katika ngome zetu,” akaeleza.

Duru zilisema baadhi ya wabunge wa ODM walidai kuwa Bw Odinga alichezewa shere katika mswada huo wa BBI kwani eneo lake wa Nyanza lilipata maeneo bunge manne pekee miongoni mwa maeneo 70 mapya yaliyopendekezwa.Kulingana na mswada huo kaunti ya Kisumu ilipata maeneo bunge mawili mapya, kaunti za Kisii na Siaya nazo zikapata eneo bunge moja, kila moja.

You can share this post!

Shughuli za ardhi kufanyika kidijitali

Madaktari walioenda Cuba warejea Kenya kuanza kazi