WANDERI KAMAU: Raila ni mdau wa kipekee katika historia ya Kenya

Na WANDERI KAMAU

WAKATI mfumo wa kisasa wa siasa ulipoanza katika ukanda wa Mashariki ya Kati karibu karne 15 zilizopita, sifa kuu ambayo ilimtambulisha mwanasiasa kama thawabu kwa falme ama jamii yake ni uzalendo.

Uzalendo ulikuwa sifa muhimu miongoni mwa wafalme na viongozi wa kijeshi, kwani ilimaanisha walikuwa tayari kujitoa kafara kwa manufaa na ustawi wa nchi zao.

Ni sifa hiyo iliyoziwezesha baadhi ya tawala maarufu kama falme za Ottoman, Persia, Saudia kati ya nyingine kuchipuka, huku nyingine zikidumu hadi leo.

Uwepo wa falme kama wa Saudia hadi sasa unatokana na msingi wa uzalendo ambao uliwekwa na waanzilishi wake katika karne nyingi zilizopita.

Ingawa msingi huo ulisambaa na kukita mizizi katika maeneo kama bara Uropa, Scandinavia na Amerika, ulichelewa kufika barani Afrika, kwani jamii nyingi ziligawanyika kwa misingi ya mipaka ziliyoweka.

Baada ya mataifa mengi ya Afrika kujipa uhuru wayo katika miaka ya sitini, kuliibuka viongozi madikteta ambao kinyume na walivyokuwa watawala wa falme za zamani, waligeuka waporaji, wasaliti na wakorofi.

Hata hivyo, kuna viongozi wachache waliobaki na kuonyesha uzalendo mkubwa kwa nchi zao licha ya masaibu, mahangaiko, dhuluma na mateso ya kisiasa waliyopitia.

Zaidi ya hayo, wameandika makumi ya vitabu kuelezea safari zao kisiasa kwa kina kuhusu yale waliyopitia. Hilo likimaanisha kuwa si wasiri wala wabinafsi, bali ni wakarimu kujenga historia za mataifa yao kwa kutofariki wakishikilia matukio hayo ya kihistoria.

Miongoni mwao ni kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.Ingawa kuna wanasiasa wengi ambao wameandika tawasifu na wasifu zao kurejelea maisha yao ya kisiasa, hakuna aliyeelezea kwa kina kama Bw Odinga.

Kufikia sasa, Bw Odinga ameandika tawasifu mbili pevu: moja ni Raila Odinga: An Enigma in Kenyan Politics (Raila Odinga: Mwanasiasa Asiyeeleweka katika Siasa za Kenya) iliyochapishwa mnamo 2006 na mwandishi Babafemi Badenjo kutoka Nigeria.

Bw Odinga pia ana tawasifu nyingine: Raila Odinga: The Flame of Freedom (Raila Odinga: Mwenge wa Uhuru) iliyochapishwa 2013 na mwandishi Sarah Elderkin.

Mbali na vitabu hivyo viwili, harakati za Bw Odinga katika siasa za ukombozi katika miaka ya themanini na tisini zimerejelewa na mamia ya wasomi wa historia kote ulimwenguni.

Baba yake Bw Odinga, Jaramogi Oginga Odinga, pengine ndiye aliyekuwa mwanasiasa wa kwanza kuandika tawasifu yake Not Yet Uhuru katika miaka ya sitini.

Ingawa makala haya hayalengi kumpigia debe Bw Odinga kwa namna yoyote ile, ukweli ni kuwa yeye ni mwanasiasa wa pekee ambaye safari yake kisiasa imenakiliwa kwa njia za kiusomi inayoweza kuvifaidi vizazi vijavyo.

Baadhi ya wanasiasa wameandika tawasifu moja moja japo hilo halitoshi.Mafanikio ya Bw Odinga yanapaswa kuwafungua macho wanasiasa kama Rais Mstaafu Mwai Kibaki, Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto kati ya wengine kuwa wana deni kubwa kwa nchi kueleza undani wa safari zao kisiasa.Ndivyo watajenga kumbukumbu itakayokumbukwa daima.

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA