KINYUA BIN KING’ORI: Twataka majibu kuhusu aliyebadilisha mswada wa BBI

Na KINYUA BIN KING’ORI

Baada ya madai kuibuka kwamba huenda kitumbua cha mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) kikaingia mchanga kwa kuibuka mswada feki uliotumwa katika mabunge ya kaunti kujadililwa, kumetokea hali ya sintofahamu na kutoaminiana katika mirengo miwili inayopigia debe mchakato huo.

Maswali ambayo Wakenya wanajiuliza bila kupata majibu ni je, ni kina nani hao waliohusika kubadilisha ripoti hiyo? Je, mswada huo ulibadilishwa katika hatua ipi?

Je, ni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyopewa ripoti hiyo ili kukagua saini na baada ya kuidhinisha kuwasilisha kwa kaunti iliyofanya hivyo?

Je, kuna mkono wa watu wenye ushawishi serikalini ambao wanapinga mpango huo japo kimyakimya waliopanga kuhujumu handisheki kwa kuvuruga rasimu hiyo?

Je, kuna vibaraka wa Naibu Rais, Dkt William Ruto ambaye amekuwa akipinga BBI, ambao walifaulu kutumia ujanja na ukora kuhakikisha ripoti hiyo imebadilishwa ili kufaulisha njama zao?

Tangu madai hayo kuibuka, tumesikia mengi yakisemwa na wanasiasa kutoka makundi mbalimbali; lile la kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga wakionekana kutoridhishwa na wenzao wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kwa kutokuwa waaminifu kwa mchakato mzima wa BBI.

Hata, wanadai wao ndio waliopanga njama hiyo.Japo mrengo wa Rais unataja mswada huo kuwa halali, na kupuuza wanaotaka ripoti hiyo itupiliwe mbali, wakisema makosa madogo ya kisarufi na uchapishaji hayawezi kuzuia mchakato huo kuendelea kulingana na ratiba yake, na tayari wabunge wameitwa kujadili mswada huo.

Yakini, hapa pana mrengo unaojaribu kuchezea mwenzake siasa chafu na usaliti. Haiwezekani kutokea makosa kama hayo na serikali inayotumia mamilioni ya pesa za mlipa ushuru kugharimia mchakato huo, ikubali mswada huo uendelee jinsi ulivyo na tayari umewasilishwa katika bunge la kitaifa na lile la seneti ili kupigiwa kura kuidhinishwa au kukataliwa.

Maadamu BBI ni shughuli inayohusu mwananchi wa kawaida, kwa nini serikali inataka kuharakisha shughuli hiyo kabla kwanza hatujabaini ikiwa kweli kulikuwa na nakala feki katika ripoti hiyo?

Mojawapo ya malengo ya BBI ni kuleta maridhiano na amani nchini na kuhakikisha viongozi, hata wa upinzani wametengewa nyadhifa serikalini, na kuwafaa vijana kuimarisha uchumi kwa kubuni nafasi za ajira zaidi na kuzalisha matumaini mapya kwa kufaulisha vita dhidi ya ufisadi.

Sasa ikiwa kuna njama na mipango ya kusalitiana, kwa uchunguzi wangu anayesalitiwa katika mpango mzima ni mdau muhimu katika mchakato huo; Raila.

Usaliti ni sumu ya haraka inayoweza kusambaratisha handisheki na kuua BBI kwa njia rahis mno.Ninatarajia wakati huu kinara wa upinzani, Bw Raila hatakubali kupumbazwa na atumike ili ripoti yenye dosari ipitishwe ili iwe rahisi kuzimwa na mahakama nao mrengo wa Rais Uhuru ujitoe lawamani kwa kusingizia uamuzi utakaotolewa na mahakama.

Ikiwa kuna kiongozi ambaye ameonyesha kujitolea kwake katika juhudi za kufaulisha mpango wa BBI, basi ni Bw Raila. Na ikiwa mashirika mwenza na kundi lake, iwe kisiri au hadharani, itafichuka kuwa wana njama za kuhujumu mpango wa BBI, basi Bw Raila anafaa kujitenga na handisheki na kuanzisha mapambano yatakayohangaisha na kutathmini utendaji kazi wa serikali ya Jubilee ambayo imesababishia taifa changamoto si haba.

Ninasitiza hivyo kwa maana ingalikuwa kweli kuna mswada feki hatua zingechukuliwa na Rais kwa kuamrisha kitengo cha ujasusi kuanzisha upelelezi kuhakikish waliohusika kukarabati ripoti hiyo wanakamatwa na kuadhibiwa kisheria.

Basi mrengo wa Balozi wa Miundomsingi wa Muungano wa Afrika (AU), Bw Raila, ujue mapema umepigwa dafrao katika BBI wanayounga mkono na badala yake wameze ukweli mchungu kwamba wamesalitiwa.

Habari zinazohusiana na hii

MAYATIMA WA BBI