• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Nani huyo kawanyonga?

Nani huyo kawanyonga?

STANLEY NGOTHO NA SIMON CIURI

MIILI ya watatu kati ya wanaume wanne waliotoweka mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado mnamo Aprili 19, ilipatikana jana imetupwa katika Kaunti za Murang’a na Kiambu.

Maiti zilizopatikana kwenye mto katika eneo la Kiharu, Kaunti ya Murang’a ni za Elijah Obuong na Jack Anyago.

Nao mwili wa Benjamin Imbai ulipatikana eneo la Gatundu Kaskazini katika Kaunti ya Kiambu. Hatima ya mtu wa nne, Brian Oduor haikuwa imejulikana kufikia jana jioni.

Mwili wa Jack ulipatikana jana ukiwa kwenye gunia chini ya daraja katika Mto Mathioya kwenye barabara ya Murang’a-Iyego-Kangema, yapata mita 50 kutoka ulikopatikana ule wa Elijah mnamo Aprili 20 katika Mto Mukangai.

Hapo jana, familia ya Elijah ilitambua mwili wa mwenda zake katika mochari ya hospitali ya Murang’a. Polisi katika kituo cha Murang’a walisema mnamo Aprili 20 walipata habari kutoka kwa wachimbaji mchanga kuwa kulikuwa na mwili kwenye gunia ndani ya mto.

Mwili huo haukuwa na nguo wala jeraha lolote isipokuwa alama ndogo ya kukwaruzwa utosini. Kisha polisi walipeleka mwili huo mochari.

Saa chache baada ya familia ya Elijah kutambua mwili wake katika mochari ya Murang’a, habari zilichipuka kuwa kulikuwa na mwili mwingine karibu na eneo ulikopatikana ule wa Elijah.

Mwandishi wa habari hizi aliweza kuutambua mwili huo ni wa Jack kutokana na picha ambazo alikuwa amepewa na familia yake awali. Mwili huo ulikuwa umetupwa katika Mto Mathioya, ambao uko mita chache kutoka Mto Mukangai.

Wachimbaji mchanga ndio walipata mwili huo na kupiga ripoti kwa chifu wa eneo hilo, ambaye aliwaomba wautoe majini.

Wakazi walisema wamekuwa wakipata miili katika mto huo, ambapo kwa mwaka mmoja uliopita wamepata maiti tano.

Mwili huo ulikuwa umewekwa kwenye gunia, na bado ulikuwa na nguo lakini bila viatu. Mikono yake ilikuwa imekatwa kabisa kiganjani. Ulipelekwa katika mochari ya Kaunti ya Murang’a.? Katika Kaunti ya Kiambu, familia ya Benjamin jana ilitambua mwili wake katika mochari ya General Kago mjini Thika.

Kulingana na rekodi, mwili huo ulipelekwa katika mochari hiyo Aprili 20 na polisi kutoka kituo cha Kiamwangi, katika eneobunge la Gatundu Kaskazini baada ya kupatikana katika Msitu wa Kieni, karibu na kituo cha biashara cha Gakoe.

Polisi walisema mwili huo haukuwa na nguo wala viatu na alikuwa na jereha mikononi lenye ishara kwamba alikuwa amefungwa pingu kabla ya kuuawa. Waliongeza pia ulikuwa na majeraha shingoni na ilionekana kama alinyongwa kwa kamba ama mikono.

Wanaume hao walitoweka Aprili 19 mwaka huu mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado muda mfupi baada ya kula nyama choma na kunywa vileo katika baa moja maarufu.

Gari jeupe aina ya Toyota Mark X lililokuwa likitumiwa na wanne hao lilipatikana umbali wa mita 500 kutoka klabu hicho.

Duru za polisi zilikuwa zimesema kuwa wanne hao walikuwa wanamulikwa na polisi kwa madai ya kuwa wanachama wa genge la watu saba waliodaiwa kuhusika katika wizi wa magari, ulaghai na utekaji nyara.

Mtu ambaye alijitambulisha kama “Erico” aliripotiwa kuambia familia za wanaume hao mitandaoni kuwa walikuwa wameuawa na polisi.

Taifa Leo iligundua kuwa wanne hao waliishi maisha ya kifahari. Hata hivyo familia zao zilikanusha walikuwa wahalifu.

“Ndugu yangu alikuwa na magari kadhaa ya kifahari aliyokuwa akikodisha lakini hakuwa mhalifu,” akasena Elvis Imbai, nduguye Benjamin.

Rekodi za polisi zilionyesha kuwa Benjamin alikuwa amehusishwa kwenye kisa cha uhalifu mnamo Januari 11 mwaka jana, ambapo majambazi walivunja gari na kuiba Sh900,000 katika kituo cha kuuzia magari eneo la Ngong Road jijini Nairobi.

Benjamin pia alikuwa na kesi katika Mahakama ya Mavoko, Kaunti ya Machakos.

Elijah naye anaripotiwa kuishi maisha ya kifahari na alipenda magari makubwa makubwa. Familia yake ilisema maisha yake ya hadhi ya juu yalifadhiliwa na jamaa zake wanaofanya kazi ng’ambo.

Duru ziliambia Taifa Leo kuwa majuzi Benjamin na Elijah waliachiliwa kwa njia ya kutatanisha katika kituo kimoja cha polisi jijini Nairobi baada ya kukamatwa kwa makossa ambayo hayakufichuliwa.

Polisi walisema mapema wiki hii kwamba wanne hao walikuwa wakitafutwa na maafisa wa usalama kuhusiana na wizi wa magari.

You can share this post!

Amerika isiilazimishe Afrika kufanya maamuzi

Msongamano wa wagonjwa wazidi hospitalini