• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Waamerika wafurahia utendakazi wa Biden siku 100 baadaye

Waamerika wafurahia utendakazi wa Biden siku 100 baadaye

Na AFP

HUKU akiadhimisha miaka 100 tangu aingie madarakani, Rais wa Amerika Joe Biden ameonekana kutekeleza ahadi nyingi alizotoa kwa raia wake na kuahidi kuzifanikisha ndani ya muda huo.

Rais Biden aliapishwa rasmi mnamo Januari 20, 2021 kwenye hafla ambayo ilisusiwa na mtangulizi wake, Donald Trump na wachanganuzi wengi wa kisiasa na wa kiuchumi wanasema kuwa, taifa hilo sasa limeanza kurejea katika mkondo unaoridhisha kiuchumi na kidiplomasia.

Ahadi ya kwanza ambayo Rais Biden alitoa ni kuhakikisha kuwa, anatoa zaidi ya dozi milioni 100 ya chanjo ya corona kwa raia wa nchi hiyo. Ameonekana kutimiza ahadi hiyo mara mbili zaidi kwa kuwa dozi milioni 220 za chanjo mbalimbali zimetolewa kwa Waamerika.

Kiongozi huyo anaonekana kufanikikisha vita dhidi ya janga hilo ikilinganishwa na wakati wa utawala wa Rais Trump ambaye alilemewa na Marekani ikawa kati ya mataifa yaliyoshuhudia maambukizi mengi.

Hata hivyo, Amerika bado ipo nyuma katika idadi ya raia waliopokea chanjo ikilinganishwa na Israel na Uingereza wanaongoza orodha hiyo.

Ingawa amekashifiwa kwa kuwaruhusu wahamiaji haramu ndani ya nchi hiyo kutoka Mexico, utawala wa Rais Biden umehakikisha kuwa wahamiaji wengi ambao wameishi Amerika, wanapata vibali na kuwa raia.

Hii ni kati ya sera ambazo zilipingwa vikali na mtangulizi wake ambaye aliwazuia wahamiaji haramu kuingia nchini humo na hata kujenga ukuta kwenye mpaka na Mexico.

Pia siku zake za mwanzo uongozini, alibatilisha baadhi ya sera kandamizi zilizowekwa na Rais Trump hasa zile zilizolenga wahamiaji wenye imani ya dini ya Kiislamu.

Uchumi wa nchi pia umeanza kuimarika kwa muda mfupi ambao amekuwa uongozini kutokana na utulivu unaoshuhudia baada ya kampeni kali mwaka jana zilizoishia katika ghasia kwenye baadhi ya majimbo.

Aidha, bunge lilipitisha msaada wa dola trilioni 1.9 ambapo kiasi kikubwa kilielekezwa kwa raia kujikwamua kutokana na maisha yao kuvurugwa kiajira na janga la corona.

Kwa kuwa chama chake cha Democrats kina wabunge na maseneta wengi katika mabunge ya uwakilishi na seneti, imekuwa rahisi mno kwa miswada ya kuboresha uchumi kupitishwa na wawakilishi hao wa raia.

Rais huyo pia ameahidi kwamba ataendelea kuboresha sekta ya afya ili raia ambao wana mapato ya chini wanayainua maisha kwa kupokea pesa kidogo za kujikimu kutoka kwa serikali.

You can share this post!

Onyo kuhusu mafuriko eneo la Ziwa Victoria

BENSON MATHEKA: Hali ya corona India ni tisho kubwa,...