• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Wasanii wa Baba Dogo watikisa anga za muziki jijini

Wasanii wa Baba Dogo watikisa anga za muziki jijini

Na WINNIE A ONYANDO

Usanii unahitaji ubunifu na uvumilivu, haijalishi utokako. Haya ndiyo maoni ya wasanii wawili chipukizi ambao wameunda kikundi kinachojulikana kama Kaiza Music Group wanatambulika sana kupitia vibao vyao vya ‘Love’ na ‘Mama Africa’ vilivyovuma sana mwaka huu.

Wasanii hao, Nashion Otieno almaarufu Nash-lee na John Owino almaarufu Slim wanasema kuwa japo wanatoka katika mtaa wa Kariadudu na Mgure huko sehemu za Babadogo, waliamua kuungana ili kutetemesha kupitia muzuki.

“Awali, tulikuwa wasanii 10 katika kikundi hiki. Kwa kuwa kila mmoja alikuwa na maono tofauti na mwenzake, tukaamua kutengana na mwishowe tukabaki sisi wawili,” walieleza Taifa Leo Dijitali.

Wakieleza jinsi maisha katika ghetto huwa mgumu, wanakiri kuwa kula, kulipa kodi ya nyumba na hata kujikimu haijakuwa rahisi kwao.

Kupitia muziki wao wa ‘Vumilia’ wanasema kuwa waliuimba wimbo huo ili kusimulia maisha magumu ya ghetto waliyopitia.

Nashion anaeleza kuwa kupitia hali ngumu ya maisha, familia yake haingeweza kulipa koodi ya nyumba na hali hii ikachangia katika kusambaratika kwa familia yao.

“Baada ya baba kufa, mama hangeweza kutushughulikia kimahitaji sisi sote wasaba. Ilibidi nihamie kwa akina John. Watoto wetu wengine hasa wa kike walilazimika kuingia katika ndoa za mapema ili waishi na wadogo wetu,” Nashion alikiri.

John naye alisema kuwa hali ngumu ya maisha ya ghetto ilimfanya kuingia katika makundi yasiyofaa hasa baada ya kuacha shule katika Kidato cha Pili.

“Kuwa kijana mmoja kati ya wasichana wanne haikuwa rahisi, ilibidi niache shule katika Kidato cha Pili ili kutafuta pesa ya kutukimu. Baba alikuwa akilewa, ikabidi nijiunge na kikundi kisichofaa,” John aliambia Taifa Leo.

John anashukuru sana uwepo, urafiki na ukaribu kati yake na Nashion ambayo imemfanya abadili mienendo yake mabaya.

“Nashion alinieka karibu naye na kunipa wosia kila mara ya kuachana na kikundi kibaya, amekuwa wa maana sana kwangu,” John alisema.

Kufikia sasa, vijana hao wawili wameandika nyimbo Zaidi ya 20 japo hazijatolewa kwa sababu ya uhaba wa pesa.

“Tunazo nyimbo nyingi sana ambazo tungependa kuwatumbuiza nao wafuasi wetu. Japo kuna studio nyingi mtaani, tunataka kutoa muziki zetu katika studio nzuri ili ngoma iweze kuvuma. Pesa pia imekuwa kizungumkuti kwetu,” walisema.

Kufikia sasa, vijana hao wawili wenye umri wa 25 wote, wameweza kurekodi nyimbo 4 ikiwemo ‘Vumilia’‘Shurbaa’‘Love’ na ‘Mama Africa’ .

Wimbo wao wa ‘Mama Africa’ waliweza kuitunga na kuiimba kwa lugha tano: Kiganda, Kiswahili, Kiingereza, Kiluhya na Kiluo.

Wimbo huo uliotolewa katika Studio ya ‘Beatz House’ na Richy Beatz ilitungwa ili kusifu asili ya Afrika na urembo wake kama kivutio kwa watalii.

Waliambia Taifa Leo kuwa japo muziki wao huchukua mdundo aina ya Afro Pop, Swahili RnB na Hip Pop, wao wanauwezo wa kuimba mdundo wowote wa muziki.

“Tunataka kuhakikisha kuwa muziki yetu inaweza kusikilizwa na watoto, vijana na hata wazee bila aibu yoyote. Hatutaki kutumia maneno machafu katika nyimbo zetu”, wawili hao waliambia Taifa Leo katika mahojiano.

Japo hawajafika kiwango wanachotaka, Nashion na John walisema kuwa wana matarajio makubwa katika ndoto yao ya uimbaji.

“Tunatarajia kung’aa katika uanamuziki panapo majaliwa. Tukipata hela, tunatarajia kufungua studio yetu binafsi na kubadili brandi yetu ya usanii,” walisema.

Kama wasanii wengine, wanaKaiza Music Group wangependa kuwa kama mwanamuziki wa RnB Bruno Mars ambaye wanasema wanapenda mtindo wake maalum wa kuimba na kucheza.

Kupitia matumizi ya mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, YouTube na Instagram, wameweza kupakia muziki wao katika mtandao na kuvutia wafuasi wengi.

Katika mtandao zote za kijamii, vijana hao wanajiita ‘Kaiza Music’. Intaneti pia imewawezesha kupata wafuasi wengi ambao hujitumbuiza kupitia muziki yao.

“Tuliweza kukutana na produsa kutoka Afrika Kusini mtandaoni ambaye alitutumia aina ya mdundo wa ngoma, kilichobakia ni sisi kuimba na kumtumia,” walisema.

“Mwanamuziki kutoka Nigeria pia tuliongea naye kupitia mtandaoni. Naye pia anadai kupiga colabo na sisi,” waliambia Taifa Leo.

Kufikia sasa, vijana hao wawili wameweza kufanikiwa kwa njia moja au nyingine. Wanasema kuwa “umbali huu, wanamshukuru Maulana”. Hijakuwa rahisi bali wanauhakika kuwa watafika tamati.

Mwaka huu, waliweza kutembele vituo kadhaa ili kuwasilisha ngoma yao ya ‘Mama Africa’ na ‘Love’ ili ziweze kutumika kama ‘Skiza Code’.

Kwa kuwa atafutaye hachoki, waliweza kufanikiwa katika Kituo cha Nation Media Group na wimbo wao wa ‘Love’ kukubalika kutumiwa kama ‘Skiza Code’.

Ngoma Vats pia ilikubali kutumia wimbo huo kama ‘Skiza Code’ mwaka huu na hata waliweza kupata Sh100 kutoka kwa Ngoma Vats.

“Kupokea Sh100 kutoka kwa Ngoma Vats ilitupa motisha sana ya kuendelea kuimba. Wengi wametamani kupata nafasi ila hawajaweza,” Nashion alisema.

“Kupitia muziki, tumeweza kuitwa mahojiano katika kituo cha redio ya KBC Radio Taifa kuhusiana na wimbo wetu wa ‘Mama Africa’, hii ilituonyesha kuwa Mungu yupo upande wetu.”

Wameweza pia kuhudhuria makao ya Nairobi Cinema mwaka wa 2009. Vijana hao wanasema kuwa japo muziki si rahisi, wanajua watapenya na hatimaye kutimiza ndoto zao.

Wanawashukuru wafuasi wao ambao  wamekuwa katika upande wao na hata kuwashika mkono na kuwashawishi hadi katika hatua ambayo wamepiga.

“Asanteni kwa subira zenu, usaidizi na maombi yenu. Hatutawaangusha, tutajikakamua na kuwafurahisha ipasavyo,” walitoa shukrani.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Buriani mhariri wetu mahiri Mauya Omauya

Loroupe ataka viatu vya utata vya Kipchoge vipigwe marufuku...