JAMVI: Mtihani wa IEBC 2022 vigogo wa siasa nchini wakiwania kuidhibiti

Na WANDERI KAMAU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inakabiliwa na kibarua kigumu kuepuka changamoto ambazo ziliandama tume za hapo awali kwenye harakati za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Licha ya juhudi ambazo zinaendeshwa na Rais Uhuru Kenyatta kuilainisha tume hiyo, wadadisi wanasema inaandamwa na changamoto tele, hasa kutokana na mivutano ya kisiasa inayoendelea baina ya viongozi wakuu nchini.

Jumatatu iliyopita, Rais Kenyatta aliteua jopo maalum la watu saba kuendesha mchakato wa kuwasaka na kuwateua makamishna wanne wa tume hiyo, kujaza nafasi nne ambazo zimekuwa wazi.

Nafasi hizo ziliachwa wazi baada ya kujiuzulu kwa makamishna wa zamani wa tume hiyo Consolata Maina (aliyekuwa naibu mwenyekiti), Bi Margaret Mwachanya, Bw Paul Kurgat na Dkt Roseline Akombe.Dkt Akombe ndiye alikuwa wa kwanza kujiuzulu mnamo Oktoba 2017, akifuatwa na wengine.

Kujiuzulu kwao kulitajwa kuchochewa na utata ulioandama marudio ya uchaguzi huo.Wanachama wa jopo lililoteuliwa na rais ni Bi Elizabeth Muli, Bw Gideon Solonka, Bw James Awuori, Bi Elizabeth Odundo, Bi Dorothy Kimengech, Bw Joseph Mutie na Bw Farudin Abdallah.

Licha ya hatua hiyo, wadadisi wanasema hata ikiwa nafasi za makamishna hao wanne zitajazwa, taswira ya IEBC machoni pa Wakenya na wanasiasa wengi si ya kukubalika, hasa baada ya utata uliokumba marudio ya uchaguzi wa 2017.

Kile kinachotajwa kujenga dhana ya kutokubalika ni uwepo wa mwenyekiti wake, Wafula Chebukati na makamishna Boya Molu na Prof Abdi Guliye.Kwa mujibu wa Bw Felix Onyango, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya chaguzi, uwepo wa watatu hao utaendelea kujenga tashwishi miongoni mwa Wakenya na wanasiasa kuhusu ikiwa tume hiyo itazingatia uwazi kwenye maandalizi ya uchaguzi.

“Tangu miaka ya tisini, changamoto kuu ambazo zimekuwa zikiandama tume za uchaguzi ni uwepo wa dhana kwamba zinapendelea baadhi ya mirengo ya kisiasa, hasa serikali iliyopo mamlakani. Dhana hiyo ndiyo imejenga matatizo yote ya kisiasa ambayo yametukumba kufikia sasa,” asema Bw Onyango.

Kulingana naye, matatizo huanza pale vigogo wa kisiasa hujenga na kueneza dhana hizo miongoni mwa wafuasi wao.Anataja hilo kuwa kiini cha machafuko ya kisiasa yaliyoshuhudiwa baada ya chaguzi tata za 2007, 2013 na 2017.

Utata

Akirejelea utata wa 2007, anasema tatizo kuu lilitokea pale aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Samuel Kivuitu, alisema hakufahamu kuhusu aliyeibuka mshindi kwenye uchaguzi huo kati ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga. Kwenye uchaguzi huo, Bw Kibaki aliwania urais kwa tiketi ya chama cha Party of National Unity (PNU).

Hata hivyo, Bw Odinga na wafuasi wake walilalamika kuhusu wizi wa kura, wakielekeza lawama zao kwa Bw Kivuitu na tume hiyo.“Kauli ya Bw Kivuitu ilizua taswira ya tume ambayo haikujiamini katika utendakazi wake.

Hilo kwa namna moja ndilo hata liliwachochea wananchi zaidi, kwani wengi walionekana kuwaamini wanasiasa wao kwamba tume hiyo ilikuwa ikiupendelea upande fulani,” asema Bw Onyango.

Wadadisi wanasema hatua ya Kenya kutorekebisha makosa yaliyojitokeza 2007 ndiyo ilichangia utata ulijirudia tena kwenye chaguzi za 2017 na 2013.

Kwa mujibu wa Bw Dismus Mokua, ambaye ni mdadisi wa siasa na masuala ya kikatiba, tume hiyo iliandamwa na dhana ya kuupendelea upande mmoja kwa mara nyingine, ndipo muungano wa CORD ukapinga matokeo ya urais.

Kwenye uchaguzi huo, muungano wa Jubilee, ulioongozwa na Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto ulitangazwa kuwa mshindi dhidi ya muungano wa Cord, uliowashirikisha Bw Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya).

“Dhana ya kuupendelea upande mmoja ndiyo iliyomfanya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK), Bw Isaac Hassan, kuondolewa kwenye wadhifa wake. Huo pia ndio ulikuwa msingi wa Cord kuenda katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi huo,” asema Bw Mokua.

Hali hiyo ilijirudia 2017, ambapo muungano wa NASA ulikataa kushiriki kwenye duru ya pili ya uchaguzi, badala yake ukimwapisha Bw Odinga kuwa “Rais wa wananchi” mnamo Januari 30, 2018 katika bustani ya Uhuru Park.

Inadaiwa mojawapo ya matakwa ya Bw Odinga kwa Rais Kenyatta baada ya kubuni handisheki mnamo 2018 ni mageuzi makubwa ya IEBC, ili kuhakikisha kutakuwa na uwazi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Wadadisi wanasema ni lazima Rais Kenyatta na vigogo wengine wajenge mazingira yatakayoipa IEBC nafasi ya kufanya maamuzi yake kwa njia huru, bila kuonekana kuingiliwa na serikali kwa namna yoyote ile.

Wanasema hilo ndilo litakaloondoa dhana ambazo zimekuwa zikiiandama kwa muda mrefu, kuhusu njama za kuupendelea utawala ulio mamlakani kwenye matokeo ya chaguzi.

“Tunaelekea katika uchaguzi mkuu wa 2022 wakati nchi inakumbwa na migawanyiko mikubwa ya kisiasa, hasa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto. Tofauti zao zimejenga taharuki kali ya kisiasa nchini kati ya wafuasi wao. Ni mwelekeo hatari, unaoweza kugeuzwa kuwa mkasa ikiwa tume itakayosimamia uchaguzi itaandamwa na dhana za kuupendelea upande mmoja,” anaonya Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.