• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Inter Milan washinda taji la Serie A kwa mara ya kwanza tangu 2009-10

Inter Milan washinda taji la Serie A kwa mara ya kwanza tangu 2009-10

Na MASHIRIKA

INTER Milan walijizolea taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka 11 mnamo Jumapili baada ya kikosi cha Atalanta kinachoshikilia nafasi ya pili kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Sassuolo.

Zikisalia mechi nne pekee kwa kampeni za Serie A msimu huu kukamilika rasmi, Inter Milan wanajivunia alama 82 kileleni mwa jedwali huku pengo la pointi 13 likitamalaki kati yao na nambari mbili Atalanta.

Inter waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Juventus kwenye kipute cha Serie A muhula uliopita wa 2019-20 huku pengo la alama moja pekee likiwatenganisha.

Kwa kuibuka mabingwa wa msimu huu, Inter wanaotiwa makali na kocha Antonio Conte wamekomesha ukiritimba wa Juventus kwenye soka ya Serie A. Juventus ya kocha Andrea Pirlo inajivunia rekodi ya kunyanyua ufalme wa Serie A kwa misimu tisa iliyopita mfululizo.

Hili ni taji la kwanza Inter tangu mwaka wa 2010 walipoongozwa na kocha Jose Mourinho kutia kapuni ubingwa wa Serie A na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Isitoshe, taji hilo ni la nne kwa kocha Conte kunyanyua katika soka ya Serie A ikizingatiwa kwamba aliwahi kuwaongoza Juventus kutawazwa mabingwa wa kombe hilo kwa misimu mitatu mfululizo kati ya 2011 na 2014. Huu ni msimu wa pili kwa Conte akidhibiti mikoba ya Inter Milan.

Katika msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Conte aliwaongoza Chelsea kutawazwa mabingwa wa kivumbi hicho mnamo 2017.

“Huu ni ufanisi mkubwa zaidi katika taaluma yangu ya ukifunzi. Maamuzi ya kujiunga na Inter hayakuwa rahisi kwa sababu kikosi hakikuwa katika hali thabiti ya kuweza kuhimili ushindani mkali na kutwaa taji lolote haraka iwezekanavyo,” akasema Conte ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Italia.

Akihojiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Italia baada ya ufanisi huo, Conte alikataa kuzungumzia mustakabali wake kambini mwa Inter ikizingatiwa kwamba angali na kipindi cha miezi 12 pekee kwenye mkataba wake wa sasa na Inter.

Inter walipoambulia sare tasa dhidi ya Udinese mnamo Januari 2021, pengo la alama mbili lilikuwa likiwatanganisha masogora hao wa Conte na watani wao wakuu AC Milan waliokuwa wakiselelea uongozini.

Tangu wakati huo, Inter walishinda jumla ya mechi 11 mfululizo na kukalia vizuri kileleni mwa jedwali. Zikisalia mechi nne pekee kwa msimu huu kukamilika, Inter tayari wamefikisha idadi ya alama ambazo Mourinho alihitaji mnamo 2010 ili kuzolea kikosi hicho ufalme wa Serie A.

Ufanisi wa Inter msimu huu umechangiwa pakubwa na uthabiti wao katika safu ya ulinzi huku mfumo wa 3-5-2 ambao wamekuwa wakitegemea sana chini ya Conte ukiwashuhudia wakifungwa mabao 29 pekee kutokana na mechi 34 zilizopita ligini.

Romelu Lukaku na Lautaro Martinez wamekuwa wavamizi wakuu wa Inter na kwa pamoja, wamefungia waajiri wao jumla ya magoli 36 kufikia sasa muhula huu.

Mwishoni mwa msimu wa 2019-20, Inter waliweka mezani kima cha Sh5 bilioni ili kujinasia huduma za beki chraf Hakimi aliyeagana na Real Madrid. Beki huyo amefungia Inter jumla ya mabao saba na kuchangia mengine saba kufikia sasa muhula huu.

Conte pia alivamia soka ya EPL na akajinasia huduma za wachezaji Alexis Sanchez na Christian Eriksen kutoka Manchester United na Tottenham Hotspur mtawalia. Beki wa zamani wa Man-United, Matteo Darmian pia alifufua makali yake kambini mwa Inter na alifunga mabao muhimu katika mechi zilizoshuhudia waajiri wake wakisajili ushindi dhidi ya Cagliari na Hellas Verona.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

JAMVI: Bunge linavyotishia kuongeza masaibu ya mswada wa BBI

Bale ashiba sifa za kocha Mason baada ya kufungia Spurs...