Serikali kutumia Sh7 bilioni kununua chanjo ya corona kufikia Juni 30

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Fedha Ukur Yatani amewaambia maseneta kwamba serikali kuu imetenga Sh7 bilioni kufadhili mpango wa ununuzi wa chanjo ya Covid-19 kutoka kwa watengenezaji mbalimbali ulimwenguni.

Alisema chanjo itanunuliwa kabla ya Juni 30, 2021 ili kuondoa hali ya wasiwasi miongoni mwa Wakenya ambao hawajapata chanjo hiyo kufikia sasa.

Tumeweka mipango ya kununua chanjo katika mwaka huu wa kifedha na mwaka ujao. Kwa mfano, katika mwaka huu wa kifedha unaokamilika Juni 30, 2021, tumetenga Sh7 bilioni. Kiwango hicho huenda kikaongezeka mwaka ujao wa kifedha wa 2021/2022,” Bw Yatani akaambia Kamati ya Seneti kuhusu Afya inayoongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito.

“Hatulengi chanjo aina moja pekee kwa sababu ya changamoto zinazotokana na uwasilishaji. Hii ni kwa sababu unaweza kuagiza leo lakini kwa sababu ya foleni ya wengine ambao pia waliagiza, huenda uwasilishaji ukacheleweshwa,” akaongeza.

Bw Yatani aliwaambia wanachama wa kamati hiyo kwamba serikali itajizatiti kupata chanjo ya AstraZeneca kwingineko ili Wakenya waliopata chanjo ya kwanza wapate awamu ya pili.

“Hii ni kwa sababu India ambayo hutengeneza chanjo ya AstraZeneca kwa wingi inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la maambukizi na hivyo imesitisha uuzaji wa chanjo hiyo kwa mataifa mengine,” Bw Yatani akasema.

Wiki jana, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kuwa Kenya inapanga kununua chanjo aina ya Pfizer inayotengenezwa Amerika na ile ya Johnson & Johnson.

Chanjo hizo zitapewa watu ambao hawakuwa wamepata chanjo ya AstraZeneca pekee kwa sababu wataalamu wanashauri dhidi ya kuchanganywa kwa chanjo.

Mnamo Machi 24, India ilisitisha uuzaji nje wa chanjo ya AstraZeneca kufuatia kupanda kwa hitaji nchini humo kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya corona.

Kufuatia hatua hiyo, jumla ya nchi 190, ikiwemo Kenya, ambayo imekuwa ikipokea chanjo hiyo chini ya mpango wa Usambazaji Chanjo ya Covid-19 katika Mataifa Masikini (COVAX) ziliathirika.

Mpango huo unaofadhiliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) pamoja na mashirika mengine, unalenga kuhakikisha kuwa chanjo ya Covid-19 inasambazwa kwa usawa mataifa yote.

Kabla ya kusitishwa kwa uuzaji nje wa chanjo, India ilikuwa ikiuza nje zaidi ya dozi 60 milioni ya AstraZeneca kwa mataifa 76.

Kenya ilipokea dozi 1.02 milioni za chanjo hiyo mnamo Machi 2, 2021.

Kufikia Jumatatu, Mei 3, 2021, jumla ya watu 887,034 walikuwa wamepokea chanjo katika awamu ya kwanza nchini Kenya, kulingana na takwimu kutoka Wizara ya Afya.

Watu hawa sasa walipaswa kuanza kupokea awamu ya pili ya chanjo kuanzia Mei 28,2021 lakini huenda wakakosa kwa sababu ya uhaba wa dawa hizo.

Wiki jana, India ilikuwa ikiandikisha zaidi ya maambukizi mapya 300,000 na zaidi ya vifo 3,000 kutokana na ugonjwa wa Covid-19 kila siku.

Ili kuzuia changamoto ya sasa ya uhaba wa chanjo ya Covid-19, waziri Yatani aliwaambia maseneta kwamba serikali iko mbioni kuwekeza katika utengenezaji wa chanjo hiyo humu nchini.

“Tutaanzisha utengenezaji wa chanjo hii kwa ushirikiano na kampuni za kimataifa jinsi inavyofanya serikali ya Rwanda,” akaeleza.